MAELEKEZO YA RC MTANDA YATEKELEZWA, HUDUMA YA MAJI YAREJEA MISASI
Kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alilolitoa Juni 07, 2024 kwa Wakala ya Maji Vijijini (RUWASA) alilowataka kuhakikisha Maji Safi yanapatikana kwenye Kata ya Misasi Wilayani Misungwi limetekeleza ndani ya saa ishirini na nne tu na sasa huduma ya maji imerejea.
Mhe. Daniel Masalu, Diwani kata ya Misasi amemshukuru Mhe. Mtanda kwa kuwatembelea kwenye kata hiyo kwani kwa sasa wana siku mbili mfululizo maji yanatoka bila kukatika na yanawanufaisha wananchi zaidi ya elfu kumi na nane kwenye kata hiyo.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwaomba wahandisi kutoka Ofisi ya RUWASA Wilaya kuhakikisha wanaendelea kutia nguvu katika kuhakikisha kunakua na uendelevu wa upatikanaji maji kwenye vituo vyote vya kutolea maji na kuhakikisha wanalinda mbiundombinu hiyo ili maji yaendelee kutoka na kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuchangia huduma hizo kwa kiasi kidogo kilichowekwa ambacho ni shilingi hamsini tu kwa ndoo ya lita 20 kwa uaminifu ili kuzipa nguvu jumuiya hizo kujiendesha na kwamba wanapaswa kuhakikisha wanaunganisha maji kwenye nyumba zao kwani gharama ni ndogo.
Ramadhani Elia, Katibu wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (MBAMIWASA) kilicho chini ya RUWASA wilaya amefafanua kuwa kwa sasa wamefanya upanuzi wa usambazaji wa maji kwa kupeleka maji kwenye maeneo ya huduma za jamii kama kituo cha afya Misasi.
"Tunamshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kututembelea maana baada ya ziara yake tumeanza kupata maji kama mnavyoona hata foleni hakuna, hali hii ni tofauti na zamani kabla hajaja kusikiliza kero zetu, tulikua na shida ya maji kwenye kijiji chetu cha Misasi." Bi. Adriana Ahmada.
Akizungumza kwa furaha mzee Mbaraka Abeid, mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Misasi amesema vijiji vya Misasi na Minawa vyenye wakaazi takribani 18500 wananufaika na huduma ya maji safi na ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kupitia kwa Mkuu wa Mkoa ambaye alitoa agizo na likatekelezwa kwa wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.