Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka wataalamu wa taaluma ya Ufuatiliaji na Tathmini kuimarisha zaidi mifumo ya kiutendaji ili kuwa kada imara.
Ametoa maagizo hayo mapema leo tarehe 11 Septemba, 2025 wakati akizindua kongamano la nne la Ufuatiliaji, tathmini na kujifunza lililowakutanisha wataalamu zaidi ya 1200 kutoka ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya mataifa 18.
Amesema ni lazima wataalamu hao wajikite katika ubunifu na kujiendeleza kitaaluma ili wapate stadi za kisasa za kusimamia miradi na kujisahihisha ili kuwa na uwajibikaji bora katika kusimamia miradi ya maendeleo.
"Kukamilika kwa mradi mkubwa wa Daraja wa JP Magufuli lenye urefu wa Kilomita 3, Meli ya MV Mwanza, Stendi za Mabasi Nyamhongolo na Nyegezi, Chanzo cha Maji Butimba, Soko la mjini kati na kipande cha Isaka -Mwanza (SGR) ni matunda ya ufuatiliaji na tathmini uliofanyika kwa kina." Mhe. Majaliwa.
Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) amesema serikali imeanzisha idara maalumu ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya serikali nchini ndani ya wizara, Sekretarieti za Mikoa na Halmshauri kama hatua za kuboresha mfumo wa sekta hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameueleza umma huo kuwa Mkoa wa Mwanza unachangia pato la taifa kwa asilimia 7.2 na kushika nafasi ya pili kitaifa na kwamba ni kitovu cha biashara kwa nchi za maziwa makuu na kwamba mkutano huo utaacha athari chanya kibiashara na kukuza uchumi.
"Ndani ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan fedha takribani Tshs. Trilioni 5.6 zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na maendeleo na uwanja wa ndege wa Mwanza upo kwenye maboresho makubwa ya kuufanya kuwa wa Kimataifa." Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.