Leo Septemba 14, 2022, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameweka Jiwe la Msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Chanzo na Kituo cha Tiba ya Maji cha Butimba Mkoani Mwanza utakaogharimu Shilingi Bilioni 69.
Akizungumza na wananchi Dkt. Mpango ameiagiza MWAUWASA kupitia Wizara ya Maji kuongeza uzalishaji wa Maji kutoka kwenye chanzo hicho na kutoishia kwenye kuzalisha lita Milioni 48 pekee kwa siku ili kupata Maji mengi zaidi na kuweza kuondoa kero ya maji kwa wananchi walio wengi hasa wanaoishi kwenye maeneo ya miinuko.
Vilevile, amewaagiza Wizara ya Maji kuhakikisha wanaunganisha huduma ya Maji ndani ya siku saba tangia kuwasilishwa kwa maombi na kuacha tabia ya kubambikiza ankara za maji zenye gharama kubwa kwa wateja tofauti na uhalisia ili kuiondolea mamlaka hiyo malalamiko kutoka kwa wananchi.
Vilevile, Makamu wa Rais amewaagiza watendaji kwenye Halmashauri kuongeza nguvu kwenye Ukusanyaji wa Mapato ya ndani na kusimamia miradi kwa umakini na Uzalendo ili iweze kuendana na thamani ya fedha zinazotumika na kuweza kuwaondolea adha wananchi.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amemshukuru Makamu Rais kwa kuwajali wananchi wa Mwanza na kuelekeza uharakishaji wa Mradi huo na amebainisha kuwa kutokana na kikao kilichoketi baina na Wizara na Mkandarasi, Mradi huo utakamilika ifikapo Disemba 2022 badala ya mwezi februari 2023 iliyosainiwa hapo awali.
Naye, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMl) Mhe. Innocent Bashungwa amesema ahadi ya kumtua Mama Ndoo Kichwani ni lazima iende sambamba na kampeni ya Usafi wa Mazingira hivyo wananchi waongeze kasi ya kufanya Usafi kwenye mazingira yao ili kuweka miji katika Mazingira safi na kuweza kutunza Afya zao.
Waziri wa Mazingira, Mhe. Dkt. Seleman Jafo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanatunza Mazingira kwa kupanda Miti na kuacha kutumia Mifuko ya Plastiki kwani mifuko hiyo inachafua vyanzo vya maji na inaharibu mitambo, hivyo wizara yake inandelea na kampeni ya kukamata mifuko hiyo ambayo hadi sasa imekamata tani 43.8.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ni sehemu ya utekelezaji wa Miradi mikubwa kwenye ukanda wa ziwa Viktoria na ulianza kutekelezwa Januari Mosi 2021 na utakamilika Mwezi Februari 2023 chini ya Mkandarasi Kampuni ya M/S Sogea Satom kutoka Ufaransa kwa Bilioni 69.
Mhandisi Sanga amebainisha kuwa Wizara imewaelekeza MWAUWASA kuongeza nguvu ya usimamizi na Mkandarasi kuongeza Rasilimaliwatu kwenye mradi huo ambao kwa awamu ya kwanza unatarajiwa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku ili ukamilike kabla ya muda na kuweza kuboresha huduma ya upatikanaji wa Maji Safi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amesema Mradi huo unatarajia kuwa suluhu ya Mgao wa Maji hasa kwa wananchi waishio kwenye miinuko kwani utaongeza lita Milioni 140 kwani hadi mwisho wa mwaka 2021 kulikua na upungufu wa Lita milioni 70 kutokana na MWAUWASA kuzalisha Lita Milioni 90 pekee wakati mahitaji ni Lita Milioni 160.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.