Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amekabidhi Dawa zenye thamani ya Tshs Milioni 27 zilizotolewa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kanda ya Ziwa (TMDA) kwa Zahanati ya Gereza la Butimba.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye Zahanati hiyo leo Juni 29, 2022 Mhe. Mkuu wa Mkoa amewashukuru TMDA kwa msaada utakaosaidia kuboresha huduma na ametoa rai kwao kuendelea kufanya ukaguzi kwa mujibu wa sheria ili wananchi waendelee kupata Dawa zilizo salama.
Aidha, amewaagiza Gereza hilo kufanya kazi kwa weledi katika kuimarisha huduma. "Tunatamani tuone huduma za afya hapa zinatolewa kwa viwango vya juu zaidi na sasa tupate mahitaji ya dawa na vifaa tiba zaidi vinavyohitajika hapa kutokana na historia ya magonjwa yanayoibuka zaidi." amesema.
"Mhe Mkuu wa Mkoa, hiki kituo hakitoi huduma kwa wafungwa pekee, kinatoa hadi kwa wananchi na wamekua wakisifiwa makamanda hawa kwa huduma nzuri na hakuna malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya huduma zinazotolewa hapa." Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi.
Akiongea wakati wa makabidhiano ya Dawa, Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki Bi Sophia Mziray amesema wao kama wadhibiti wa ubora, ufanisi na Usalama wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi wanaamini dawa hizo zitasaidia kuongeza huduma kwenye Zahanati hiyo.
"Kwa siku tunahudumia kati ya wateja 60 hadi 80 na tumekua na changamoto ya dawa kadhaa kwenye kituo chetu hivyo kwa kupata dawa hizi itatusaidia sana kuongeza huduma kwa wafungwa na wananchi." Dkt Ramadhani Kinyunyi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.