Matokeo Utafiti wa Afya ya Uzazi, Mtoto na Viashiria vya Malaria 2022 yaje na Mageuzi chanya kisekta: RAS Mwanza
Leo Februari 7, 2024 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amefungua semina ya siku mbili ya utoaji wa matokeo ya Utafiti wa afya ya Uzazi na mtoto na Viashiria vya Malaria mwaka 2022 na kuwataka washiriki kuyatumia vizuri matokeo hayo ili yawe na tija kwenye sekta ya afya.
Akizungumza kwa niaba yake kwenye ukumbi wa mikutano Hotel ya Monarch, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu, Daniel Machunda amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya maboresho makubwa sekta ya afya hivyo changamoto za vifo vya mama na mtoto viepukike kwa kutumia matokeo ya utafiti huo.
Amewataka washiriki hao wengi wao wakiwa ni wataalamu wa afya kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa,kutambua kuwepo na vifo vinavyotokana na uzazi vinachangia kupunguza nguvu kazi ya Taifa na mipango ya maendeleo kwa ujumla.
"Naumia sana ninaposikia kumetokea kifo cha mama na mtoto, hili ni jambo jema (Uzazi) na lenye furaha ndani ya familia la mama kujifungua lakini lisije na taarifa mbaya, nawasihi sana ndugu washiriki baada ya semina hii mkalete mageuzi ya kweli kwenye maeneo yenu," amesisitiza Machunda kwenye ufunguzi.
Ameipongeza Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa utafiti huo na hasa katika eneo la afya ambalo lina umuhimu wa pekee ndani ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
"Kanda yetu ya Ziwa licha ya kufanya vizuri wajawazito kuhudhuria kliniki kwa asilimia 91 lakini idadi ya wanaokwenda kujifungua kwenye vituo vya afya hairidhishi,pia utoaji wa chanjo tumefikia asilimia 51 tofauti na Ile inavyotakiwa na Serikali ya 53%, yote haya hatuna budi kwenda kuyafanyia kazi,"Katibu Tawala Msaidizi.
Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Emilian Karugendo amesema Taifa lolote Duniani haliwezi kuwa na maendeleo kama litakabiliwa na changamoto ya wananchi wake kuwa wagonjwa,kwa kutambua umuhimu huo Ofisi yake kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara za afya Bara na Visiwani wamefanya utafiti huo na kutoa taarifa kwa Serikali kwa hatua zaidi.
Washiriki wa semina hiyo ni waganga wakuu wa mikoa,waganga wakuu wa wilaya,waratibu wa Malaria,na Maafisa mipango kutoka mikoa ya Mwanza,Shinyanga,Mara,Geita,Kagera na Simiyu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.