Serikali ya awamu ya Sita imepongezwa kwa kuendelea kuwa sikivu na kuyafanyia kazi maslahi ya Wafanyakazi licha ya kuwa na changamoto za Uchumi ulioutikisa Ulimwengu hivi sasa.
Akizungumza katika Sherehe za Wafanyakazi, Mei Mosi zilizofanyika ki-Mkoa Mkoani Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe Mhandisi Robert Gabriel amesema maombi kadhaa waliyotoa Watumishi Mei Mosi ya mwaka Jana iliyofanyika Kitaifa Mkoani Mwanza yamepatiwa ufumbuzi.
"Tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwani mbali ya kupunguziwa makato ya Kodi kutoka asilimia tisa hadi nane pia malimbikizo ya Mishahara,Watumishi kupandishwa madaraja pia Mikopo isiyo na riba ni miongoni mwa hatua zilizotekelezwa ambazo zimeongeza ari ya uwajibikaji" amesema Mhe. Mhandisi Gabriel.
Ameongeza kuwa, Wafanyakazi waendelee kuzingatia nidhamu na utii kazini kwani bado maslahi yao mengine yanaendelea kufanyiwa kazi na yatakuja na majibu chanya wakati utakapowadia.
Aidha, amewakumbusha Waajiri wote Mkoani Mwanza kuzingatia na kutekeleza Sheria za kazi na malipo stahiki yanalipwa kwa wakati hasa Sekta binafsi.
Pamoja na hayo, Mhe Gabriel amewahimiza Wakazi wa Mkoa wa Mwanza kushiriki kikamilifu Sensa ya Watu na Makazi itayofanyika Agosto 23 mwaka huu ili Taifa liweze kutekeleza Mipango ya Maendeleo kikamilifu.
Sherehe za Mei Mosi Kitaifa Mwaka huu zimefanyika Mkoani Dodoma Mgeni Rasmi akiwa ni Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.