Zaidi ya asilimia 90 ya watu wenye umri wa miaka kati ya 30 hadi 50 wanaopatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu chanzo chake bado hakijulikani mpaka sasa.
Aidha, watu wenye umri wa chini ya miaka 30 na zaidi ya miaka 55 chanzo cha wao kupatwa na ugonjwa huo kinajulikana na kikiondolewa tatizo linakwisha.
Takwimu hizo zilitolewa na daktari bingwa wa magonjwa ya figo na shinikizo la damu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Ladislaus Rudovick.
Alisema ugonjwa wa shinikizo la damu umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni msingi (primary) na sekondari (secondary).
Katika siku ya Shinikizo la Damu Duniani, hospitali ya Bugando ilitoa huduma za upimaji afya bure kwa magonjwa yasiyoambukizwa.
Dk.Rudovick alisema kila tatizo la kiafya linatibika ikiwa mgonjwa akiwahi kupata matibabu .
Alivitaja baadhi ya visababishi vya ugonjwa huo ni pamoja na mishipa ya kwenye figo kuwa miembamba, uvimbe tumboni na matatizo ya tezi yanayosababisha homoni mwilini kuongezeka pamoja na mfumo wa maisha.
Kwa mujibu wa Dkt. Rudovick, mfumo wa maisha unaweza kuwa chanzo kikubwa hasa kwa watu wenye kipato kizuri kinachowafanya kula ulaji usiopangiliwa pamoja na kukosa muda wa kufanya aina yoyote ya mazoezi, japo ya kutembea.
“Utakuta mtu anatoka ndani kwake na kuingia kwenye gari hadi ofisini. muda wa kazi ukiisha anaingia tena kwenye gari, anapita sehemu za burudani, anaagiza nyama, tena ile nyekundu na kileo, hasa bia, kisha anarudi nyumbani anaoga na kulala na kesho yake hivyo hivyo,” alisema
Alisema suluhisho la kwanza kwa mtu mwenye tatizo la shinikizo la damu ni kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiopangiliwa huku akitoa tahadhali wanaotumia tiba asilia ambazo hazijafanyiwa utafiti.
Dk. Rudovick, alisema tiba asili zisizofanyiwa uchunguzi zinasababisha madhara mengine yanayoweza kusababisha matatizo ya kiafya ikiwemo kuharibu figo.
Katika maadhimisho hayo pia uchunguzi wa magonjwa ya ngozi ulifanyika huku, Dk. Nelly Mwageni akisema kwamba magonjwa hayo nayo huendana na umri wa mtu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.