Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana na marafiki zake kwa msaada wa Madawati 105 kwa shule za Msingi Nyehunge na Mtakuja zilizopo Wilayani humo.
Akizungumza mbele ya kamati za Shule hizo zilizopo Halmashauri ya Buchosa,Mkuu huyo wa Wilaya amesema huo ni mfano wa kuigwa kwa watu wengine kuona umuhimu wa kujitoa pale unapokuwa na nafasi kuchangia Maendeleo ya Taifa letu.
"Balandya amesoma shule hii ya Nyehunge kwa kutambua umuhimu wa elimu ameona ni vyema atoe mchango huu wa Madawati haya ambayo yatachangia watoto wetu kusoma katika mazingira bora na hatimaye kuwepo na ufaulu mzuri wa masomo" amesema Mhe Ngaga.
Awali akizungumza kwa niaba ya Bw. Balandya Elikana, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimaliwatu Bw. Daniel Machunda amebainisha msaada wa Madawati hayo ni kuuunga mkono kwa vitendo Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imejikita kuendeleza elimu nchini kwa kila mtoto aweze kupata nafasi ya kusoma.
Bw. Machunda amesema awamu ya kwanza February mwaka huu Balandya akishirikiana na wafanyakazi wenzake aliofanya nao kazi Idara ya Menejimenti ya Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango walifanikisha utengenezaji wa Madawati 120 yaliyogawiwa shule za Msingi Nyehunge,Bukiliguli na Ng'wabasabi,Madawati ambayo yamewanufaisha wanafunzi kati ya 210 hadi 315.
"Tumeona dhamira ya dhati ya Rais wetu katika kuleta maendeleo kwa kuondoa michango shuleni na wanafunzi kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi cha Sita na kuziboresha shule zote za Serikali,tunapoonesha kuunga mkono jitihada zake tunazidi kumpa ari ya kuwapigania wananchi wake kusonga mbele katika nyanja zote ikiwemo kielimu na kiuchumi" amesisitiza Machunda.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa Julius Mlongo amesema kata ya Nyehunge ina jumla ya shule 10 za Msingi kati ya hizo 8 zinamilikiwa na Serikali na 2 ni za binafsi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw Balandya Elikana amesoma shule ya Msingi Nyehunge kuanzia mwaka 1978 na kihitimu elimu ya msingi mwaka 1984.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.