Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa amewaahidi wananchi wa Wilaya ya Magu vituo vya afya, maji, barabara na umeme na kuwataka kuchagua viongozi makini watakaoleta maendeleo.
Ametoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Kijiji cha Kisamba Kata ya Lubugu na Irungu Kata ya Nyigogo wilayani Magu akiwa njiani kuelekea jijini Mwanza akitokea mkoani Mara.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imefanya mambo makubwa ya kuhudumia jamii na kuleta maendeleo chini ya Rais Mhe.John Magufuli, hivyo waichague tena CCM kwa miaka mingine mitano kwa sababu ina uwezo wa kuratibu mambo yote na inatambua changamoto za wananchi wake.
“Mhe.Rais Dkt. Magufuli amefanya makubwa ya kuhudumia jamii katika sekta za afya,elimu, maji na barabara kazi ambayo ni ya miaka mitano na tutaifanya tena, kwa sababu sera yetu ni maendeleo mpeni miaka mitano migine afanye maendeleo makubwa ya nchi hii,”alisema Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa Magu bado kuna changamoto ya vituo vya afya, serikali itajenga vingine ingawa imekamilisha vituo vya afya Kahangara (sh. bilioni 1.4), Lugeye (sh. milioni 400) na Kabila (sh.milioni 400) ambapo kituo cha Kahangara kitaongezewa sh. milioni 400, pia itatoa sh. milioni 200 za upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu.
“Tumejenga vituo vya afya vya kimkakati vyote vina huduma zote ambapo kutokana na mahitaji ya dawa kuongezeka tumetoa sh. bilioni 10.8 ili kuwezesha upatikanaji wa dawa ili wananchi wasiendelee kununua kwenye maduka binafsi,”alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM na kusisitiza;
“Huduma za matibabu ni bure kwa wazee, watoto chini ya miaka mitano na huduma ya kujifungua kwa akina mama wajawazito, kama kuna watendaji wanakwamisha wanawatoza fedha hao ni wauaji, kama fedha zipo kwa nini uwatoze fedha, twambieni wachukuliwe hatua.”
Mhe. Waziri Mkuu pia alisema serikali iko kwenye mchakato wa kutekeleza muswada wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote wapate matibabu na itatoa magari ya kubeba wagonjwa mahututi na wa dharura hasa wajawazito kwenye vituo vyote vya afya nchini vikiwemo vya Wilaya ya Magu.
Aidha alisema endapo wananchi wa Magu wataichagua CCM mkakati wa serikali ni kuhakikisha wilaya hiyo inapata maji ya uhakika na tayari imepeleka shilingi bilioni 23 .3 za miradi ya majina kufafanua kuwa mradi wa maji kwenye vijiji vya Kinango (Sh.milioni 107),Matela (sh.milioni 397),Kabale (sh.milioni 231),Buhumbi, Bugatu, Ndagalu, Nyasato (sh. bilioni 2.1) na Nsolo (sh.Bilioni 1).
Pamoja na hayo pia aliahidi kujenga miundombinu ya barabara za makao makuu ya wilaya kwa kiwango cha lami ambapo kwa Magu imetenga mabilioni ya fedha za ujenzi wa barabara za Bujora, Magu-Ngudu, Shishani hadi Simiyu.
“Umeme bado kwenye vitongoji na mitaa, vyote vitapata na utafungwa hata kwenye nyumba za tembe kwa sh. 27,000, nguzo bure hadi nyumbani. Kwenye kilimo cha pamba tunataka kujenga viwanda vya kuchambua pamba tuingie kwenye na kuzalisha nyuzi,”alisema Mhe. Majaliwa.
Aliongeza kuwa serikali imefanya kazi kubwa kwa miaka mitano na kwenye uchaguzi wa mwaka huu anatafutwa kiongozi makini mwenye uwezo wa kusimamia serikali yake na kuwaunganisha watanzania.
Mhe.Majaliwa amedai anatakiwa kiongozi wa kukomesha rushwa inayoathiri maendeleo atakayeweza kuwahudumia wanyonge na kusimamia rasilimali za nchi ziwanufaishe wananchi wote.
" Tunayo sababu ya kumpigia kura Mhe.Rais Dkt.Magufuli, amefanya kazi kubwa, maendeleo hayana chama ndo maana nimekuja kumwombea kura ameongoza nchi yenye watu zaidi ya milioni 60 yenye makabila mengi na wenye itikadi ya vyama tofauti,hivyo tumpe tena miaka mingine mitano ili afanye maendeleo mengine zaidi," alisema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga alisema wananchi wa Magu kwa miaka mitano wamepata mafanikio mengi hivyo wana haki ya kumpa kura Mhe.Rais Magufuli Oktoba 28, mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.