MILIONI 300 ZA MAPATO YA NDANI ZAUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI WA BUDUSHI -KWIMBA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla Shaibu Kaim ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi, uongozi wa Kwimba na wananchi kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya uliozingatia ubora na viwango kwenye kijiji cha Budushi.
Ametoa pongezi hizo mapema leo Julai 19, 2023 kwenye Uwekaji wa jiwe la msingi la kituo hicho ambacho kinatekelezwa kwa zaidi ya milioni 315, zikiwemo milioni 300 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ambacho ujenzi wake umeanzishwa na wananchi wa kijiji cha Budushi kwa kununua eneo la hekari saba pamoja na kuchimba na kujenga msingi kwa gharama ya zaidi ya milioni 15.
"Ukitaka kujua kwamba Mhe. Rais Samia anafanya kazi kubwa kwenye sekta ya afya basi njoo ujionee Sumve, ukienda katika vijiji cha Bumengeja, Nyamikoma, Mwashilalage kote kazi za heshima sana zinaendelea na hapo awali wananchi hawakuwahi kupata huduma hizi karibu na makazi yao." amesema Mhe. Kasalari Mageni, Mbunge wa Sumve (CCM).
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji, Ndugu Emanuel Lameck ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Sumve amefafanua kuwa asili ya juanzishwa kwa ujenzi wa Kituo hicho ni kutokana na wananchi kuchoshwa na adha ya msongamano wa wagonjwa kwenye Hospitali inayomilikiwa na Kanisa katoliki Sumve.
Ndugu Lameck amefafanua kuwa ujenzi wa kituo hicho unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yanajengwa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na choo cha nje chenye matundu manne ambavyo kwa pamoja ujenzi wake umefikia 90% na kwamba kwenye awamu ya pili wanatarajia kujenga wodi za wanawake na wanaume na kichomea taka.
"Mradi huu unatakiwa kukamilika Julai 30, 2023 na kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi wapatao 72,138 ambapo kata ya Sumve ni wananchi 19,195, Mantare 13,153, Ngulla 13,673, Walla 19,763 pamoja na Mwabomba wananchi 3,192." amefafanua Mtendaji Kata.
Katika wakati mwingine Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ameipongeza Kwimba kwa kuanzisha shamba darasa la malisho ya mifugo ambapo wafugaji watapata ujuzi wa kupanda, kutunza na kuhifadhi malisho na mbegu ili kuongeza nalisho ya mifugo na kupunguza migogoro kwa wakulima na wafugaji pamoja na kusaidia kuhifadhi mmomonyoko wa ardhi.
Kwenye Kijiji cha Ibindo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru amefungua mradi wa maji ambao tayari zaidi ya wananchi 105 wameshaunganisha maji ya bomba kwenye makazi yao na akatoa wito kwa viongozi kusimamia sheria za utunzaji na uhifadhi wa mazingira zinazozuia shughuli zote za kijamii kwenye vyanzo vya maji na akatoa majuma mawili kuondolewa kwa mazao yaliyolimwa ndani ya mita 60.
Baada ya Kuzindua Shamba la hekta 105 lenye aina Tisa za Miti Malya linalomilikiwa na Jeshi la Magereza huku likigharimu zaidi ya Milioni 489.1 Kiongozi wa Mbio za Mwenge ameagiza ukamilishaji wa viwango wa Barabara ya Lami nyepesi yenye urefu wa Kilomita 1.36 kuanzia Sokoni-DAS House inayojengwa na M/S Jassie and Company LTD (JASCO) kwa zaidi ya Milioni 631.7 chini ya Usimamizi wa TARURA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.