MIRADI YA ZAIDI YA SHS BILIONI 2 YAKAGULIWA H/YA BUCHOSA,RAS MWANZA ATOA MAAGIZO
Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema imepewa maagizo ya kuharakisha miradi ya maendeleo na pia kusimamia na kufuatilia miradi ya vijana inayotokana na mikopo ya asilimia.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 13,2024 na Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana alipofanya ukaguzi wa baadhi ya miradi yenye thamani ya zaidi ya shs bilioni mbili na kusisitiza ni lazima ikamilike kwa wakati ili iwe na tija kwa wananchi.
Akiwa kwenye kituo cha afya Nyakasungwa kilichogharimu shs milioni 250 fedha zilizotokana na mapato ya ndani lakini bado hakijaingiziwa umeme na maji,mtendaji huyo wa Mkoa amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Benson Mihayo kukaa na Taasisi husika ili kukamilisha haraka.
"Hiki kituo ni lazima kiwe na maji muda wote na pia akiba ya maji kutokana na aina ya kazi yake,fanyeni utaratibu wa kuvuna maji ya mvua ili kujiwekea akiba,"Balandya.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inazidi kuiboresha sekta ya afya hivyo anaamini kwa juhudi za halmashauri hiyo kituo hicho kitakuja kutoa huduma bora kwa wananchi
Kuhusu miradi ya vijana inayotokana na mkopo wa asilimia kumi amevipongeza vikundi vinavyofanya vizuri na kurejesha fedha kwa wakati lakini akawakumbusha Maafisa mipango kuweka utaratibu wa kuwasimamia vyema ili fedha hizo za mkopo ziwanufaishe na wengine.
Aidha amemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Senyi Ngaga kuwaelimisha wananchi kutumia maji safi na salama waliyowekewa na Serikali baada ya kupata taarifa ya baadhi ya wananchi kutoyapenda maji hayo na kuyatumia yale yasiyo salama kwa madai yaliyowekewa dawa ya kuuwa vijidudu hayana ladha.
Katibu Tawala huyo anaendelea na zoezi la kukagua miradi ya maendeleo na Septemba 14,2024 atakuwa Halmashauri ya Sengerema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.