MIUNDOMBINU BORA YA SHULE YAONGEZA HAMASA YA UANDIKISHAJI WANAFUNZI NYAMAGANA
*Uandikishaji wa wanafunzi wavuka matarajio shule za awali na msingi*
*RC Makalla amshukuru Rais Samia kwa Ujenzi wa madarasa*
*Shule mpya ya Kanenwa yawapunguzia watoto adha kutembea umbali mrefu*
*RC Makalla aagiza umeme na maji kupelekwa kwenye shule mpya*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amekagua miundombinu ya elimu ya awali, msingi na sekondari wilayani Nyamagana pamoja hali ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo amebaini kuwa ujenzi wa miundombinu bora umepelekea uandikishaji wa wanafunzi kuvuka lengo la matarajio
Akiongea katika nyakati tofauti wilayani humo leo tarehe 09 Januari 2024, Mkuu wa Mkoa amesema matokeo ya usajili wa wanafunzi yanatokana na nia njema ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha miundombinu kwenye shule za msingi na sekondari inaimarika ili kuwa na mazingira mazuri ya kujifunza na kujifunzia.
Kutokana na ujenzi wa shule mpya ya msingi Kanenwa Mhe. Makalla amebainisha kuwa si tu imevunja rekodi ya uandikishaji kwa wanafunzi wa awali (Maoteo 150, walioandikishwa 350) na darasa la kwanza (Maoteo 200, waliosajiliwa 250) bali itaondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda kwenye shule za Bujingwa na Bukaza.
"Leo ni siku ya pili tangia shule zifunguliwe, kuanzia walimu, uongozi wa kata na wilaya, wazazi na walezi nisisitize tuweke msukumo, ushawishi na ufuatiliaji wa wanafunzi waweze kuripoti shuleni." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa akiwa kwenye shule ya sekondari Mirongo ambayo wameripoti watoto 71 kati ya 223.
Vilevile, Mhe. Makalla ameongeza kuwa shule zote mpya ndani ya Mkoa huo zimesajiliwa na hali hiyo itasaidia kuwa na wigo mpana wa watoto kupata shule za jirani na akatumia wakati huo kuwaagiza TANESCO na MWAUWASA kupeleka huduma kwenye shule mpya ili kutoa fursa kwa wanafunzi na walimu kuwa na mazingira mazuri ya ujifunzaji na kufundishia.
Wakati akitoa pongezi na shukrani kwa Rais Samia kwa kuhakikisha elimu inakua bora nchini, Makalla amewapongeza uongozi wa wilaya na Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miundombinu hususani ya madarasa ya ghorofa na kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni kwa wakati mara tu muhula mpya wa masomo ulipoanza mapema wiki hii.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe. Stansilaus Mabula ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais kwa kumwaga pesa nyingi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya elimu na kuwapongeza watendaji wote ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ushirikiano uliopelekea ukamilishaji bora wa miundombinu ya shule.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.