Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amezitaka taasisi zote zenye miundombinu rafiki ya michezo mkoani humo kuacha ubinafsi na kushirikiana na wadau wa michezo pale wanapohitaji kutumia miundombinu hiyo kwa maendeleo ya sekta hiyo.

RC Mtanda ametoa wito huo leo Desemba 21, 2025, alipokuwa akifunga Mashindano ya Rolling Stone Championship 2025, yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Nsumba Jijini Mwanza.

Amesema michezo kwa sasa ni sekta inayokua kwa kasi duniani, ikiwa na mchango mkubwa katika uchumi kwa kuzalisha ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hivyo inahitaji kuungwa mkono kwa vitendo.

Akizungumzia mashindano hayo, RC Mtanda amesema Rolling Stone Championship 2025 ni jukwaa muhimu la maendeleo ya michezo nchini kwa kuwa yanalenga kuibua, kukuza na kulea vipaji vya vijana wenye umri wa miaka 9 hadi 21, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa michezo kikanda.

Mhe. Mtanda ameahidi kuyasimamia mashindano hayo ili mwaka ujao yafanyike kwa mafanikio makubwa zaidi na kushirikisha kikamilifu nchi za Afrika Mashariki na Kati.

“Mwanza ni kitovu cha nchi za Maziwa Makuu, hivyo mashindano haya yana nafasi kubwa ya kuwa mashindano ya kweli ya Afrika Mashariki na Kati,” amesema.

Aidha, RC Mtanda amezitaka shule na taasisi zote zenye miundombinu ya michezo kuacha uchoyo na kuwakaribisha wadau wa michezo wanaohitaji kutumia maeneo hayo kwa shughuli za michezo.

“Niwapongeze uongozi wa Shule ya Nsumba kwa ushirikiano wao. Kama wasingewapkea na mngeweka makazi nje, gharama zingekuwa kubwa. Huu ni mfano wa kuigwa,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa African Sports Park Centre, Bw. Hamis Alli, ambaye pia ni mratibu wa mashindano hayo, amesema Rolling Stone Championship ilianzishwa mwaka 2000 ikishirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Amesema kwa mwaka 2025, mashindano yameshirikisha Tanzania pekee, yakiwa na jumla ya timu 25 kutoka vituo 14 vya kulea na kukuza vipaji vya vijana.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.