MKANDARASI DARAJA LA MABATINI ATAKIWA KULIKAMILISHA KWA WAKATI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Aprili 10, 2025 amekagua ukarabati wa Daraja la Mabatini unaofanywa na kampuni ya Nyanza Roads Work na kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha ndani ya muda aliyopewa wa mwaka mmoja.
Akizungumza na mkandarasi huyo pamoja na wananchi katika eneo la ujenzi la Mabatini wilayani Nyamagana, Mhe. Mtanda amesema hatovumilia ucheleweshaji endapo halitakamilika mwishoni mwa mwaka huu.
"Tayari nimesikia mkandarasi umeshalipwa na Serikali fedha za utangulizi Tshs. Milioni 600 na makubaliano ya mkataba ni muda wa mwaka mmoja hivyo nataka kuona Novemba mwaka huu kazi hii iwe imekamilika', amesema Mtanda.
Aidha, amebainisha kuwa eneo hilo ni barabara kuu ya kwenda mikoa ya Mara na Simiyu hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwacheleweshea shughuli za kiuchumi wananchi na amewataka Wakala ya Barabara TANROADS kusimamia kwa karibu kazi hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambroce amesema ukarabati wa daraja hilo umegharimu zaidi ya Tshs bilioni 6.3 na licha ya changamoto ya hali ya hewa hivi sasa ya mvua lakini watahakikisha mkandarasi huyo anafanya kazi hiyo usiku na mchana ili aikamilishe kazi hiyo kwa wakati waliyokubaliana.
"Ukarabati huu umeigharimu miundombinu yetu kuhamishika kazi ambayo imesababisha kuwepo na ukosefu wa maji siku za nyuma lakini hivi sasa hall ya upatikanaji wa huduma ya maji imerejea kama kawaida kasoro maeneo machache ya pembezoni mwa Jiji kutokana na kazi ya kutandaza mabomba inaendelea', Nelly Msuya,Meneja MWAUWASA mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.