Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa rai kwa wafanyakazi wa taasisi na idara za serikali mkoani humo kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na weledi ili kuuletea maendeleo Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa baada ya kupokea maandamano ya azimio la kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi kutoka kwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani humo.
"Twendeni tukafanye kazi kwa uzalendo, itatuletea heshma kwa Mungu na kila mmoja akitekeleza majukumu yake tutakua tumemrudishia shukrani Mhe. Rais kwa vitendo na tusionekane kwenye wizi, ubadhirifu wala rushwa na haki ikainue maisha yetu."
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewashukuru wafanyakazi hao kwa utashi wao kuthamini mema aliyoyafanya Mhe. Rais kwao kupitia utumishi wao na kwa pamoja wakaamua kutoa kauli ya kumpongeza kwa maandamano yenye furaha na bashasha.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi amesema Serikali ya awamu ya Sita itaendelea kuwa sikivu hivyo ni wajibu wa kila mfanyakazi kufanya kazi kwa bidii katika eneo lake.
Akisoma risala ya Wafanyakazi Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoani Mwanza TUCTA,Zebedayo Athuman amesema shukurani ya Wafanyakazi kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ni kuchapakazi kwa bidii kwa lengo la kuliletea Maendeleo Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Mkoani Mwanza,TUCTA Yusuph Simbaulanga ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha Wafanyakazi kitendo kitakachoongeza ari ya kazi.
Vilevile, Mhandisi Gabriel amewasihi viongozi wa wafanyakazi kushughulikia mara moja changamoto za wafanyakazi na kuwasilisha kwake zile zinazohitaji msaada zaidi wa ofisi yake na akaahidi kutoa ushirikiano.
"Kwa mema yote haya yaliyofanyika tunalo deni kwa Mhe. Rais hivyo niwaombe viongozi wa shirikisho na viongozi wa vyama vya wafanyakazi isiwepo kero ya mfanyakazi yeyote bila kuifanyia kazi na kama kuna changamoto yoyote nitaifanyia kazi ili mfanyakazi yeyote akifika asubuhi kazini aanze kwa sala ya shukrani kwa mwenyezi mungu." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.