Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella ameagiza kuundwa timu ya wajumbe watakaosaidia kusimamia sera bora ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Agizo hilo limetolewa jijini Mwanza wakati wa mkutano na wadau wa sekta hizo uliolenga kujadili hali, mwenendo na mafanikio yake kimkoa.
Timu hiyo yenye wajumbe kutoka sekta husika inatarajiwa kuandaa na kusimamia Mwongozo bora utakaosaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kupiga hatua kiuchumi na hatimaye kuchangia pato la mkoa na taifa kwa ujumla.
"Tunaenda kuunda timu ya wajumbe watakaotusaidia kuandaa mwongozo wa njia bora za kufikia mafanikio kwenye sekta hizi na tutaweka wazi mawasiliano yao ili kama mtu ana maoni ya maboresho ya sekta hizi muhimu basi awasiliane nao na niwahakikishie tutafanyia kazi maoni ya kila mtu atakayoleta kwetu.
"Kwa hiyo kwa wenzetu mliopo kwenye nafasi ya uandaaji mbegu au uchakataji mazao yote nanyi pia fanyieni kazi mawazo ya wakulima maana wao ndio wanaelewa hali halisi, wapeni nafasi wasikilizeni na msijifanye mnajua kila kitu.
"Kama ambavyo tumekubaliana sasa ni wakati wa vitendo, tunatoka kwenye nadharia tunaenda kufanya kazi, tunataka matokeo chanya yaonekane kwa mkulima, mfugaji na mvuvi wetu.
"Muda wa kukaa tunaongea tu umekwisha, tumefanya majaribio kwenye pamba na tumeona tunao uwezo wa kusukumana tukafika, kwenye mifugo tumejitahidi lakini bado, sasa tuhamishie nguvu pia kwenye mpunga na alizeti ndani ya misimu miwili natajia kuona uzalishaji unaongezeka mara dufu", Alisema Mongela.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi Bodi ya Pamba Tanzania, James Shimbe alisema kuwa ni wakati sasa wa kuwa na kilimo chenye tija hasa kwenye pamba, kwani ni wazi kuwa takwimu zinaonyesha uzalishaji wa mazao unaongezeka japo manufaa kwa mkulima yamebaki kuwa siyo makubwa.
" Kwa muda mrefu kilimo nchini kwetu kimeonekana hakina tija kwa sababu tumezoea kufanya uzalishaji ambao hauna tija, lakini mabadiliko tunayaona baada ya kuanza kutoa semina kwa wakulima wetu.
"Mfano msimu huu uzalishaji umeongezeka baada ya wakulima waliokuwa hawazalishi kwa tija kuwafikia na kuwapa mafunzo ya uzalishaji na uvunaji wenye tija lakini mbali na kuzalisha kwa tija hivi sasa ifikie hatua kuwe na malipo ya nyongeza ya thamani hasa kwa wakulima wanaozalisha mazao yenye thamani zaidi ya moja hasa wakulima wa pamba ambayo inatoa nguo pamoja na mafuta hivyo mnunuzi anafaidika mara mbili au zaidi kumbe na mkulima anatakiwa anufaike vivyo hivyo",Alisema Shimbe.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafugaji Mkoa wa Mwanza (UWAWAMWA), Rehema Mwalugala aliiomba Serikali kutenga aridhi ya kutosha kwa ajili ya malisho ya mifugo ya kisasa na yale ya kawaida.
"Sisi kama wafugaji Mkoa wa Mwanza tupo kwenye mipango ya kuunda vikundi ili tuweze kukopesheka kiurahisi pamoja na kukuza ushirikiano kati yetu na taasis za serikali.
"Ila niiombe serikali itutengee maeneo ya kutosha kuendesha shughuli zetu kwani mbali na kuwa sekta yetu ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa lakini bado ushirikiano tunaopewa na taasisi za serikali hauridhishi," alisema Rehema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.