Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella ameiamuru Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuwasilisha mikataba ya miradi ya maji ya Sangabuye na Igogwe- Nyafula- Kabusungu kutokana na kutoridhishwa na utekelezaji wake.
Mhe. Mongella pia ameagiza wakandarasi wa mradi ya maji ya Igogwe- Nyafula- Kabusungu, kampuni za D4N, Jasco na Makimu nao kufika ofisini kwake haraka wakiwa na mikataba yao.
Amri hiyo ameitoa wakati wa ziara yake kutembelea miradi ya maji ya Sangabuye na Igongwe iliyopo katika manispaa ya Ilemela na Mradi wa Lwanhima uliopo katika wilaya ya Nyamagana.
“Kesho mniletee mikataba ofisini kwangu pamoja na taarifa kamili ya hali ya mradi, mje tuijadili...haiwezekani zaidi ya miaka minne hakuna kinachoendelea. Hapa hata ukaguzi inaonekana ilikuwa haufanyiki. MWAUWASA inaelekea hamjaanza kuifanyia kazi miradi mliyokabidhiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema Mhe. Mongella.
Katika kituo cha maji cha Lwanhima, Mhe. Mongella amemuagiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kwamba transfoma inafungwa katika mradi huo na kwamba atakwenda kukagua utekelezaji huo baada ya siku 10 kuanzia leo
“Tarehe 30 nitakuwa hapa kushuhudia transifoma ikifungwa. Tena Mkuu wa wilaya andaa kabisa mkutano wa hadhara na wananchi siku hiyo. Nitakuja hapa tangu asubuhi na tutasubiri hapa mpaka transifoma ifungwe,” alisema Mkuu wa mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.