Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amemtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Chanzo Kipya cha Maji eneo la Butimba kuongeza bidii ya ujenzi ili kukamilisha kwa wakati na uweze kuwanufaisha wananchi wanaosubiri mradi huo.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo leo Septemba 08, 2022 wakati akikagua mradi mkubwa wa cha Chanzo Kipya cha Maji eneo la Butimba unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mazingira Mwanza (MWAUWASA) huku ukijengwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S Sogea Satom kutoka Ufaransa kwa gharama ya Tshs. 69,337,520,300 ambao ulianza kutekelezwa Februari Mosi 2021 huku ukitarajiwa kukamilika Mwezi Februari 2023.
Aidha, amesema amefurahishwa sana na Utekelezaji wa mradi huo mkubwa na amewaagiza viongozi wa wilaya ya Nyamagana kuhakikisha utakapokamilika mradi huo wa maji uliofikia asilimia 40 ya utekelezaji kuhakikisha unawanufaisha wananchi wa eneo linalozunguka mradi huo kabla ya kusambaa kwenye maeneo mengine.
Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyera amesema mradi huo mkubwa wa kisasa umegawanyika kwenye maeneo kadhaa yakiwemo Tanki kubwa, eneo la kuondoa madini tofauti, eneo la kubadilisha tabia ya maji, chemba ya kuondoa matope, eneo maalum la kuchuja maji, eneo la kuuwa wadudu na eneo la usafirishaji na kwamba hatua hizo zithakikisha ubora na usalama wa maji kuwa wa juu.
"Mradi huu wa Ujenzi wa Chanzo kipya na kituo cha kusafisha Maji safi cha Butimba utakapokamilika kwa awamu hii ya kwanza utazalisha lita elfu 48 kwa siku hivyo utaboreshwa huduma ya upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wapatao 450,000 katika Jiji la Mwanza kutoka Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwamina, Fumagila, Sawha, Igoma, Kishiri na Nyamanoro, aidha maeneo ya Usagara, Nyashishi na Fella katika wilaya ya Misungwi na Kisesa, Bujora na Isangijo katika Wilaya ya Magu yatanufaika pia." Mhandisi Msenyera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.