RC MTANDA AWATAKA WANUFAIKA TASAF KUWEKA MALENGO KUPITIA FEDHA WANAZOPOKEA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wanufaika wanaopokea fedha za Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kuweka malengo kupitia fedha wanazopata ili waweze kujikwamua na umaskini ambapo ndio lengo la msingi la mradi huo.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo leo Februari 20, 2025 alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mradi huo katika Kijiji cha Shigumulo Kata ya Mwang’halanga Wilayani Kwimba ambapo amewata wanufaika hao kujiwekea malengo ili waweze kuhitimu umaskini.
“Msaada huu ipo siku utakoma, ni lazima uwe na mipango, anzisha hata mradi wa kuku ambao utakusaidia kusomesha watoto, kuendesha familia na mwisho wa siku uweze kuhitimu kutoka kwenye mradi huu”.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewapongeza Wanufaika hao ambao kundi kubwa alilokuatana nalo ni Wanawake na kuwataka kuwekeza katika kufanya kazi kwa bidii hata kupitia miradi ambayo TASAF imekuwa ikiibua ikilenga kuwawezesha Wanufaika hao pia kama vile ujenzi wa barabara, uchimbaji wa visima, mabweni au madaraja.
“Mtumie miradi hii kujikwamua na mbadilishe maisha yenu, fedha mnazozipata msiende kuzinywea pombe maana mradi utakwisha na wewe utakuwa umekwisha”.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ngw’ilabuzu Ludigija amewataka Wanufaika hao kuchukua wosia wa Mkuu wa Mkoa kwa kuwa aliyoyaeleza yote yana uhalisia na hawana budi kuyafuata.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.