Mikoa ya Mwanza na Mara inaongoza kwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo nchini kwa kuwa na juu ya asilimia 30.
Akiongea kwenye uzinduzi wa kampeni ya ugawaji dawa za kukinga na kutibu magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika Mkoa wa Mwanza Oscar Kaitaba Afisa Mpango wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Kutoka Wizara ya Afya alisema Mikoa hiyo inamaambukizi makubwa kwa sababu wadudu wanaoeneza ugonjwa wanazaliana kwa wingi.
“Wananchi wa kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza na Mara wanatabia ya kujisaidia pembezoni mwa ziwa, wanachota maji ya kutumia ziwani na sio tu kwa ajili ya wadudu kuzaliana sana lakini pia na zao la mpunga linachangia kuwepo kwa maambukizi ya magonjwa haya”alisema Kaitaba.
Naye Mratibu wa magojwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Mwanza, Mabai Thobias alisema, walengwa ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi kumi na nne ambao wapo mashuleni ambapo kwa mkoa wa mwanza ni zaidi ya watoto 878,624 kwenye shule 663 za mkoa wa huo.
“Walengwa wetu ni watu 627,917 katika kata 41 za Halmashauri za Ukelewe, magu, Ilemela, Buchosa na Mwanza mjini ambao tutawatembelea kaya moja baada ya nyingine ili kukamilisha ugawaji dawa baada ya kugawa kwa wanafunzi mashuleni”alisema Thobias
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Emmanuel Kipole alisema, kwa mujibu ya tathimini ya awali kupitia Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu, NIMR kituo cha Mwanza, kwa kushirikiana na Mradi wa udhibiti endelevu wa kudhibiti kichocho katika jiji la Mwanza wa mwaka 2018 katika Halmashauri za Ilemela na Nyamagana, kati ya watu 2,148 wenye umri wa miaka 15 na Zaidi waliofanyiwa uchunguzi 1,748 sawa na 81,4% walikutwa na maambukizi ya kichocho.
“Kutokana na kiwango hicho cha maambukizi na kwamujibu wa tafiti na maelekezo ya kitaalamu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) jamii inapaswa ipewe dawa ya kukinga na kutibu hivyo, Mkoa unawajulisha wananchi na wakazi wote kuwa tarehe 6 agosti mwaka huu tutaendesha kampeni za ugawaji dawa wa kukinga na kutibu magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho kwa umri wa kwenda shule, waliopo na wasiokuwepo shuleni,” alisema Kipole.
Mhe Kipole aliongeza kuwa, dawa hizo zinatakiwa mtoto awe amekula chakula ndani ya masaa yasiyozidi mawili na baada ya kula ndo apatiwe dawa hizo na kuwa chakula kiandaliwe shuleni siku hiyo ya kumeza dawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.