MWANZA NI SEHEMU SAHIHI YA UWEKEZAJI - RC MTANDA
Serikali ya Mkoa wa Mwanza imewakaribisha na kuwahakikishia ushirikiano wa dhati Wawekezaji na Wafanyabiashara wote wanaotamani kuja kufanya biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Mwanza ikiwa ni kwa mustakabali wa kukuza biashara na uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 10, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alipokuwa akifungua Semina ya uhamasishaji wa masuala ya ushindani yenye lengo la kumlinda mlaji wa bidhaa bandia kwa wazalishaji wa Jiji la Mwanza, ambapo amewashukuru Tume ya ushindani (FCC) kwa kufungua Ofisi ya Kanda Mkoani Mwanza.
Mkuu wa Mkoa amesema kwa kufungua Ofisi katika Mkoa wa Mwanza inaongeza juhudi, kuleta huduma karibu na wananchi na kufanya utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa sheria hususani katika masuala ya ushindani, udhibiti wa bidhaa bandia na kumlinda mlaji kwa ujumla.
“Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi iliyofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 Mkoa wa Mwanza una jumla ya watu 3,699,872 Idadi hii ya watu ni fursa katika masoko na biashara ukizingatia pia Mkoa wa Mwanza ni wa pili kwa idadi ya watu ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam”.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema kiuchumi Mkoa wa Mwanza unachangia kwenye pato la Taifa (GDP) kwa Trilioni 13.59. ukiwa ni Mkoa wa Pili kwa kuchangia kwa asilimia kubwa kwenye pato la Taifa, ambapo Mkoa wa Mwanza unachangia kwa asilimia 7.2.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda ameeleza kuwa uchumi wa Mkoa wa Mwanza unachangiwa na Kilimo 75% (mazao, mifugo na misitu); huduma 10% (biashara, hoteli, usafirishaji, mawasiliano, taasisi za kifedha, kodi za pango, elimu, afya, na utawala); Uvuvi 7% na viwanda na ujenzi 8% (madini, umeme, maji, ujenzi na uzalishali).
“Nimeelezea uchumi wa Mkoa kwa uchache na takwimu si kwa sababu mimi ni bingwa wa Takwimu, hapana, bali nimefanya hivyo ili muweze kupata picha halisi ya uchumi wa Mkoa lengo likiwa mkiwa kama sekta ya biashara kwa pamoja muone namna bora ya kuzitumia vizuri fursa za kiuchumi zilizopo”.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa amewaomba FCC haswa walio katika Kanda ya Mwanza kushirikiana pamoja na kwa ukaribu ili kuhakikisha masuala ya kiushindani yanasikilizwa na yanatatuliwa kwa wakati na wananchi wanapewa elimu zaidi kuhusu masuala ya ushindani, kumlinda mlaji na mapambano dhidi ya bidhaa bandia.
kabla ya kufungua semina hiyo Mkuu wa Mkoa amewataka wafanyabiashara waliopata fursa ya kuhudhuria semina hiyo kwenda kuitumia vizuri elimu watakayopata na kuwa mabalozi wazuri wa FCC katika kuwaelimisha wafanyabiashara, wazalishaji wenye viwanda wengine na wananchi kwa ujumla ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.