MWANZA TAYARI KUUPOKEA MWENGE WA UHURU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameutangazia umma kuhusu mapokezi ya mbio za mwenge Mkoani humo unaotarajiwiwa kupokelewa Oktoba 06, 2024 katika Kijiji cha Nyamadoke kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ukitokea Mkoa wa Geita.
Mhe. Mtanda ametoa taarifa hiyo mapema leo Oktoba 01, 2024 kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya mkuu wa mkoa alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri 8 kwa umbali wa kilometa 627.
Aidha RC Mtanda amesema Mwenge wa uhuru 2024 ukiwa Mkoani Mwanza utafikia jumla ya miradi ya maendeleo 58 inayogharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 99,370,447,286.76 ambapo kati ya hizo wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamechangia milioni 2,615,713 576.00.
"Kati ya fedha hizo Halmashauri zimechangia milioni 2,775,384,864.08 huku Serikali Kuu bilioni 19,704,775,674.99 na washirika wa maendeleo bilioni 74,274,573,171.69". Amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameendelea kwa kusema Mkoa wa Mwanza umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, wiki ya Vijana na miaka 25 ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 199-2024.
"Kwa umuhimu huu ninawaomba wananchi wote mjitokeze kwa wingi ili kuulaki mwenge wa Uhuru pamoja na kushiriki katika maadhimisho hayo". Amesema Mhe. Mtanda.
Kilele cha Mbio za mwenge wa uhuru kitafanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba mnamo tarehe 14 Oktoba2024 kuambatana na Kongamano la Vijana litakalofanyika tarehe 11-12 Oktoba 2024 kuanzia saa moja asubuhi katika ukumbi wa Rock City Mall.
Sambamba na hayo Mdahalo wa kumuenzi Baba wa Taifa utafanyika tarehe 13 Oktoba 2024 katika Ukumbi wa Rock City ambapo tukio hilo litakuwa mubashara kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu ni "Tunza mazingira, "Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.