Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewataka Viongozi katika ngazi zote kuanzia kwenye Vitongoji kushirikiana kwa dhati kutekeleza Miradi ya Maendeleo kwenye maeneo yao shabaha ikiwa kuondoa changamoto zinazoikabili jamii.
Amesema hayo leo Julai 22, 2020 wakati wa Mkutano wa Wadau kuelekea Kampeni kubwa ya Ujenzi wa Miundombinu ya Vyumba vya Madarasa inayokwenda kuanza wiki ijayo Mkoani humo katika kuhakikisha wanafunzi kwenye shule za Msingi na Sekondari wanasoma kwenye madarasa bila kusongamana.
"Umoja ni nguvu, tunataka tuone kwenye majira haya ya mwanzo kabisa mwa mwaka wa fedha tunaazimia kwa pamoja kuwatoa watoto wa Shule za Msingi na Sekondari kwenye msongamano madarasani kwa kujenga vyumba vya madarasa vya kutosha." Amesisitiza.
Akifafanua suala la Elimu Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa huo kwa shule za Msingi una Mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa zaidi ya elfu 18 na huku vilivyopo ni vyumba elfu 7 na kufanya kuwe na upungufu wa vyumba vya madarasa zaidi ya Elfu 11 ikiw ni sawa na asilimia 59 huku Halmashauri ya Nyamagana ikiongoza kwa upungufu.
Vilevile, amebainisha kuwa kwa Shule za Sekondari Mkoa huo una upungufu wa zaidi ya vyumba vya Madarasa zaidi 750 na kwamba hali hiyo imemfanya kuitisha Mkutano huo Mkubwa wa Wadau kuhakikisha wanaweka Mkakati wa pamoja ili kumaliza tatizo hilo mara moja.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndugu Ngusa Samike amebainisha kuwa Watendaji wote wako tayari kwa zoezi hilo nyeti na kwa hakika Mkoa unakwenda kulitekeleza kwa muamko mkubwa kwenye kila Halmashauri ili wanafunzi watakaoanza masomo mwakani watakupa mapinduzi makubwa sana kwenye suala la Miundombinu.
"Nikuhakikishie Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa Wabunge wote tumejipanga na tupo tayari kukuunga mkono kwenye kampeni hii, tutaenda kama timu na hakika Mwanza tunaanza safari hii leo na kwa hakika miezi sita baadae hatutakua sawa na sasa", amesema Mbunge Nyamagana, Mhe Stanslaus Mabula.
Mhe. Simon Mpandalume Diwani kutoka Magu ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Mkoa amemshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kuja na Kampeni hiyo na amemhakikishia kuwa Waheshimiwa Madiwani wapo tayari kushirikiana naye kwa dhati katika kufanikisha adhma hiyo ya kizalendo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waheshimiwa Wabunge, Taasisi za kifedha, Kamati ya Amani, Mabenki, Marafiki wa Mkoa, Wachimbaji wa Wauza Madini pamoja na Waziri wa Maji (MB) Mhe. Jumaa Aweso ambaye yupo kwenye ziara ya kukagua Miradi ya Maji Mkoani humo na amechangia Mifuko 200 ya Saruji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.