Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Daniel Machunda ameongoza mazoezi ya pamoja kwa watumishi wa umma na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mazoezi hayo yamefanyika katika Viwanja vya Furaisha Wilaya ya Ilemela, yakishirikisha viongozi mbalimbali wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya Jiji la Mwanza.

Akizungumza baada ya kuongoza mazoezi hayo, Bw. Machunda amewapongeza washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha moyo wa kujali afya zao.

Amewasisitiza wananchi na watumishi wa umma kuendelea kushiriki mazoezi mara kwa mara akibainisha kuwa mazoezi ni msingi muhimu wa afya bora na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

“Afya njema huanzia kwa mtu binafsi. Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kuimarisha mwili, akili na kuongeza ufanisi kazini,” amesema Bw. Machunda.

Aidha, amewataka watumishi wa umma pamoja na wananchi kutoka taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kujitokeza kushiriki mazoezi ambayo hufanyika kila siku jioni kuanzia saa 12:00 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake, Afisa Mnadhimu Namba Moja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi SACP Gideon Msuya amewapongeza washiriki kwa kujenga utamaduni wa mazoezi na kueleza kuwa shughuli hiyo imechangia kuimarisha ushirikiano, kutambuana baina ya taasisi mbalimbali pamoja na kubadilishana uzoefu wa kimazoezi.

Ameongeza kuwa mazoezi ya pamoja yanaimarisha mshikamano na mahusiano mema kati ya vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi, jambo linalosaidia kudumisha amani na usalama katika jamii.

Mazoezi hayo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Mwanza wa kuhamasisha jamii kuzingatia afya bora kupitia mtindo wa maisha wenye mazoezi, lishe bora na kuepuka tabia hatarishi zinazochangia magonjwa yasiyoambukiza.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.