**Wiki ya madini Mwanza yaja na mwarobaini wa madini chumvi*
*
Maonesho ya wiki ya madini yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza kuanzia Mei 3 hadi 9, 2023 yamekuwa na faraja kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya chumvi nchini baada ya kupitishwa kwa maazimio 14 ya kuendelea sekta ya madini ikiwemo madini hayo.
Akizungumza jijini hapa jana baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania(Femata) John Bina alisema maazimio hayo yamepitisha na wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo, wiki ya madini na kongamano la madini lililofanyika Mei9,2023.
“Tumepitisha maazimio 14 kati ya hayo maazimio 10 yameilenga serikali kupitia Wizara ya Madini na manne yanailenga Femata yote yatafanyiwa kazi ili kuwanufaisha wachimbaji,miongoni mwa maazimio ni wizara ya Madini
kuandaa mkutano mkuu wa kitaifa utakaojadili changamoto na fursa zilizopo kwenye uchimbaji na biashara ya madini ya chumvi nchini.
“Madini haya yamesahaulika sana, licha ya umuhimu wake kwenye mwili wa binadamu lakini yamekuwa hayapewi kipaumbele wakati tunayo mengi hapa nchini hivyo tunaamini hatukukaa hapa Mwanza kwa kwa siku nane bure siku hizo zitazaa matunda,” alesem Bina na kuongeza
“Wachimbaji wa madini hayo na wafanya biashara watakwenda kunufaika kwa sababu serikali ikitambua changamoto na fursa zilizopo kutoka kwa sisi wachimbaji itazifanyia kazi maana serikali yetu inatusikiliza siku zote sisi wachimbaji wadogo na lengo letu la la kuchangia pato la taifa kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2028 tutalifikia,”alisema Bina
Maazimio mengine yaliyopitishwa ni pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kuendelea kufanya utafiti wa madini kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini na taarifa za tafiti ziwafikie wadau kwa wakati, mchakato wa utoaji leseni kwa wachimbaji wadogo uwe wa wazi na unaozingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuendana na haki kwa wachimbaji wadogo wanaoomba leseni kupitia Tume ya Madini.
Pia Wizara ya Madini kukamilisha zoezi la kupitia tozo zinazotozwa na halmashauri kwa wachimbaji wadogo ili isiwe kikwazo katika uchimbaji mdogo wa madini .
Aidha Bina aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Mwanza inayoongozwa na Mhe. Adam Malima kwa usalama waliopata muda wote wa siku tisa walipokuwa mkoani humo .
Mgeni rasmi aliyefunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania, (TAWOMA) Taifa Semeni Malale, alisema ili Femata iweze kutimiza malengo iliyojiwekea ni vyema wanachama wote wakashirikiana na kusameheana huku wakifanya shughuli zao kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.