Mkoa wa Mwanza umezindua kampeni ya umezeshwaji wa dawa za kukinga na kutibu ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto walio na umri kati ya miaka 05-14 huku wakiwa na malengo ya kuwapatia dawa hizo watoto zaidi ya laki saba katika shule zipatazo 955 za msingi ili kukabiliana na asilimia 84 ya watoto wanaodhaniwa kuwa na maambukizi hayo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa kampeni za kitaifa hususani ni katika magonjwa ambayo hapo awali yalikuwa hayapewi kipaumbele lakini sasa serikali imeamua kwa dhati kukabiliana nayo.
“Magonjwa haya kimsingi hudhorotesha sana afya za watoto na hii nikutokana na asili ya watoto kupenda kucheza katika maji au kupita katika maji pasipo kuwa waangalifu, alisema Mkuu huyo wa mkoa na kuongeza kwamba, kutokuwa na afya njema hupekea hata nguvu kazi ya uzalishaji kupungua, kutokana na kutokuwa na watu watakao shiriki shughuli za maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa amesema, kutochukua tahadhari za mapema, nguvu kazi nyingi huishia katika kujitibu jambo linalochukua rasilimali watu, muda na fedha kwaajili yakuangalia afya hapo badae, hivyo zoezi linalofanyika kwa sasa nikuliepusha taifa na madhara makubwa ya badae.
“Rasilimali fedha zinazo tumika wakati wa ugonjwa zingeweza kutumika na mgonjwa mwenyewe au familia kufanya shughuli za maendeleo” aliongeza Mongella.
Mwisho mkuu huyo, amemalizia kwakusema, kwa upande wa watoto hupunguza sana uwezo wao katika masomo lakini pia katika suala la michezo, hivyo kuyataja kama magonjwa yenye hasara kubwa katika jamii yetu.
Awali akitoa maelezo ya utangulizi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Leonard Subi, amesema usugu wa magonjwa mengi ya utu uzima chimbuko lake ni kutokana na kutochukua tahadhari za mapema.
Subi amesema tafiti zinaonesha kuwa watu katika mwambao wa ziwa Viktoria wamekuwa waathirika wakubwa wamagonjwa hayo, huku akizitaja Wilaya za Magu, Ilemela, Nyamagana Sengerema na Buchosa pamoja na Ukerewe katika mkoa huu kuwa waathirika wakubwa.
“Takribani ni watoto asilimia 84, wameambukizwa kichocho pamoja na minyoo huku kichocho kikitajwa kuwa juu zaidi ya minyoo” amesema Subi na kuongeza kuwa, Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapatiwa dawa za minyoo na zoezi la safari hii sio zoezi lakwanza.
Subi amesema, wagonjwa wengi zaidi ya asilimia 80 wanaofika hospitalini kwaajili ya maradhi ya saratani ya kibofu cha mkojo historia inaonesha waliwahi kuugua kichocho walipokuwa wadogo, “Mhe. Mkuu wa mkoa Kichocho pia kinaweza kuathiri mfumo mzima wa ubongo” hivyo tunaomba watoto tuwaangalie na wakati mwingine tuwe mstari wa mbela katika kuwakataza na michezo ya kwenye maji.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Dkt. Angelina Mabulla katika salaam zake zilizo tolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, ameunga mkono zoezi hilo, huku akisema kuwa watoto ndio nguvu kazi ya taifa la kesho hivyo tunakila sababu yakuzingalia na kuzilinda afya zao wangali wadogo, “Taifa lisilo wekeza kwa watoto wake ni taifa mufilisi” alisema Mabulla.
Mkoa wa Mwanza, umefanya zoezi hilo, huku ukiwa umesambaza dawa hizo katika vituo vyote vya afya pamoja na shule zote 955 za msingi kwenye mkoa wa Mwanza huku wakiwa na lengo lakuwafikia watoto zaidi ya laki saba waliopo shuleni na wale ambao wapo majumbani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.