Ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito,watoto chini ya miaka 5 ,watu waliopata ajali na wenye uhitaji , Mkoa wa Mwanza umeandaa mpango mkakati wa kukusanya chupa za damu 1,359.
Hayo yamebainishwa na Mratibu huduma za maabara na damu salama Mkoa wa Mwanza Shigella Julius alipokuwa akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amesema watakuwa na Kampeni ya robo mwaka hivyo mpango huo wa kukusanya damu utafanyika kuanzia Desemba 14 hadi 18 mwaka huu .
Ameongeza kuwa damu salama ni huduma muhimu sana katika kuokoa maisha ya binadamu wenye uhitaji wa damu huku makundi maalumu yanayohitaji sana damu salama ni akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5, Watu wanaopata ajali, na watu wenye magonjwa kama seli mundu(Sickle cell).
Aidha, amesisitiza kuwa damu inapatikana kwa binadamu mwenyewe kwa kujitolea ili kuokoa maisha ya binadamu mwingine, kwani hakuna kiwanda kinachotengeneza damu hivyo uchangiaji wa damu ni tendo salama linalosimamiwa na wataalamu wenye mafunzo maalumu.
"Damu inapotolewa haiendi moja kwa moja kwa mgonjwa, inapitia mchakato wa kupimwa magonjwa kama HBV, HCB, Kaswende na VVU kuna makundi manne (4) ya Damu, “A”, “B”, “AB” na “O”na kila moja lina chanya na hasi Mchangia damu anaweza kuwa mwanaume au mwanamke na umri kuanzia miaka 18 hadi 60 uzito kuanzia kilo 50 mwenye afya njema asiye na magonjwa kama shinikizo la damu, Kisukari,"amesema Julia's.
Pia kwa upande wa Mwanamke atachangia damu baada ya miezi 4 na mwanaume baada ya miezi 3
mchangia damu atapitishwa kwenye fomu yenye maswali mbalimbali ili kuona kama anazo sifa za kuchangia damu, mchangia damu atafanyiwa vipimo vya awali kama wingi wa damu, msukumo wa damu “blood pressure” na uzito.
Akielezea faida za damu amesema ni kuokoa maisha ya binadamu mwenzako, ni tendo la huruma, upendo na ni tendo la ibada na kuufanya mwili ujisikie vyema, hivyo kuna timu 10 za kukusanya damu, ambapo timu 8 ziko katika Halmashauri zote nane na timu 2 ziko katika Hospitali za rufaa ya Mkoa Sekou Toure na rufaa ya kanda Bugando.
" Vituo vinavyotoa huduma ya damu katika Halimashauri 8 za mkoa huu ni 42 ,pia makusanyo ya damu kuanzia robo tatu zilizopita ambazo ni January hadi September mwaka huu ni 15,414 sawa na asilimia 66.6 ambapo lengo letu lilikuwa ni 23.133"ameeleza Julius.
Amesisita kuwa wamepewa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala, pia uwepo wa timu za kukusanya damu katika kila Halmashauri na Hospitali za Rufaa za Kanda na Mkoa na
kufanikisha maadhimisho ya siku ya mchangia damu Duniani, kampeni zilianza Juni1 hadi14 mwaka huu na kufanikiwa kukusanya chupa 1,961 (218%) ya lengo la chupa 900, na (145.3%) ya lengo la Mkoa chupa 1,350 .
"Tumeshika namba 1 Kitaifa kufanikisha kampeni ya robo ya Julai – Septemba, 2020 kwa kukusanya chupa za damu 1,363 (100.9%) ya lengo la chupa 1,350 na kuongoza katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa,Kukusanya chupa za damu 493 katika maadhimisho ya siku ya Kisukari Dunia yaliyofanyika wiki ya pili ya Novemba, mwaka huu pia uanzishwaji wa magroup ya Whatsap ya Mkoa ni msaada mkubwa" ameeleza Julius.
Hata hivyo kumekuwa na mwitikio mdogo wa wananchi kujitolea kuchangia damu pamoja na upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha huduma ya kukusanya damu pia baadhi ya timu kutokuwa na vitanda maalumu vya kulala wachangia damu.
Hivyo mkakati wao wa kutatua changamoto hizo ni kuendelea kufanya uhamasishaji kwa njia mbalimbali, kuzihimiza Halmashauri na hospitali ya Mkoa kuendelea kutenga fedha ya kutosha na kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Halmashauri kutenga fedha ya kununulia vitanda maalumu katika bajet ijayo.
"Naomba tushirikiane kwa namna mbalimbali katika kufanikisha kampeni hii na hata baada ya kampeni kauli mbiu “TOA ZAWADI YA UHAI MSIMU HUU WA
SIKUKUU KWA KUCHANGIA DAMU” maana ya kauli mbiu hii, inaonesha umuhimu wa jamii kushiriki uchangiaji wa damu wa hiari ili kuokoa maisha ya wagonjwa wote wenye uhitaji wa damu. Pia ni tendo la kibinadamu la kuwashirikisha wagonjwa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Tutuba amesema kuwa Mkoa unajipanga ili kuhakikisha unakuwa mfano katika uchangiaji damu kwa hiari hivyo amewaasa watumishi kujitokeza kwa wingi ili kuchangia na kuokoa maisha ya wahitaji wa damu.
" Sisi kama Mkoa tutakuwa na Kampeni ya watumishi wote mlango kwa mlango ili kuhakikisha kila mtumishi mwenye sifa za kuchangia anachangia, tutapanga siku yetu rasmi tutawajulisha watumishi wote" amesema Tutuba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.