Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuinua kaya zenye changamoto ya umasikini kwa kuzijengea uwezo,uelewa na kuziwezesha kukuza uchumi na kuboresha vipato ambapo imetenga sh. bilioni 24.595 za kutekeleza mradi wa kupunguza umasikini mkoani Mwanza.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.Mhandisi Robert Gabriel, wakati akizindua awamu ya nne ya mradi huo miaka mitano wa kupunguza umasikini mkoani humu.
Alisema adhima na dhamira ya serikali ya awamu ya sita ni kuinua kaya zenye changamoto ya uchumi na kuziwezesha kutumia fursa za kuongeza kipato,kukuza uchumi wa kaya,kuboresha huduma za jamii na kuwekeza kwenye maendeleo ya watoto.
Mhe.Mhandisi Gabriel alisema mpango huo wa miaka mitano, kitaifa ulizinduliwa mkoani Arusha, Oktoba 10, mwaka huu, na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Mohamed Mchengerewa, utatoa ajira za muda kwa kaya za walengwa,itaibuliwa miradi ya miundombinu ya jamii ya kutolea huduma za afya,elimu,barabara,maji safi na salama pamoja na utunzaji wa mazingira.
“Miradi hiyo itatoa ajira za muda kwa jamii na kupata fedha za kuboresha maisha,kuongeza kipato na kuendeleza miundombinu ya afya,elimu na maji,kupata ujuzi na stadi za maisha kwa walengwa,”alisema.
Mhe. Gabriel alisema kuwa wasimamizi wakuu wa miradi hiyo kutoka mkoani waisimamie kwa kufuata miongozo yote ili kuendana na fedha zilizotolewa ambazo kitakuwa kipimo cha uadilifu na uwajibikaji.
“Tumepewa zaidi ya sh. bilioni 24 kutekeleza miradi ya kupunguza umasikini,naomba tuipongeze serikali na juzi tu Mwanza tumepokea bilioni 22 za kujenga madarasa, hurum ya mama n serikali yake anastahili pongezi nyingi sana maana tumeletwa mzigo wa kutosha hatujawahi kuupata hadi usingizi unakataa,”alisema Mhandisi Gabriel.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladslaus Mwamanga,alisema Mradi huo wa Kupunguza Umasikini Tanzania (TPRPIV) ni dirisha la kuongeza fedha kwenye mapungufu ya miradi ya miundombinu ya afya,elimu,maji na barabara zitakazotumiwa na jamii, ambayo itatekelezwa kwenye mikoa mitano ya Njombe,Arusha,Geita,Mwanza na Simiyu.
Alisema madhumuni makubwa ya kutekeleza mpango huo wa awamu ya 4 ni kupunguza umasikini wa wananchi ili watu waende kwenye vituo afya kujiimarisha kiafya na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa madarasa na nyumba za watumishi ili kuziba mapengo katika maeneo mengine ya mradi.
“Kutakuwa na miradi ya ajira,vitaanzishwa vikundi vya watu 15 na kupewa sh. milioni 15 za kuanzisha miradi ya kujiongezea kipato, na hiyo ndiyo mikakati ya TASAF na ndio maana ya kujenga uelewa wa pamoja kati ya viongozi wa serikali,wanasiasa na watalaamu ili wafikishe ujumbe sahihi kwa wananchi waje na vipaumbele vyao,”alieleza Mwamanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.