MWANZA YAPOKEA MWENGE WA UHURU, KUKIMBIZWA KWENYE MIRADI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA BILIONI 21
Leo Julai 13, 2023 Mkoa wa Mwanza umepokea Mwenge wa Uhuru kwenye Kijiji cha Muluseni wilayani Ukerewe ukitokea Mkoani Mara ambapo unatarajiwa kukimbizwa kwa takribani Siku 8 kwa umbali wa Kilomita 813.4 nchi kavu na majini.
Akipokea Mwenge huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema ukiwa Mkoani humo unatarajiwa ambapo ukiwa Mkoani humo unatarajiwa kukimbizwa kwenye miradi 51 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 21.
Mhe. Makalla amesema Mwenge wa Uhuru Mkoani humo unatarajiwa kuweka Mawe ya Msingi kwenye miradi 17 yenye zaidi ya Bilioni 13.7, kufungua 9 ya zaidi ya Bilioni 3.5, kuzindua 15 kwa Bilioni 3.1 huku ukitarajiwa kutembelea miradi 10 iliyogharimu Milioni 609.2.
CPA. Makalla ameongeza kuwa, kwa mwaka 2022 Mwenge wa Uhuru Mkoani Mwanza ulitembelea jumla ya Miradi 52 yenye thamani ya Bilioni 18.7 na kwamba kwa mwaka 2023 Mwenge huo utatembelea Miradi 05 iliyowekewa mawe ya Msingi mwaka jana kwa ajili ya kuifungua.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Abdalla Shaib Kaim ameomba ushirikiano kwa Mkoa wa Mwanza hususani usahihi wa taarifa za miradi na nyaraka ili kufanikisha mbio za Mwenge huo kwa mwaka 2023.
Wakati huohuo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Hassan Bomboko kwa ajili ya kuukimbiza kwenye miradi 6 ya wilaya hiyo kwa siku ya kwanza ya tarehe 13, Julai, 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.