Serikali mkoani Mwanza imewakutanisha maofisa elimu wilaya, kata na wakuu wa shule kwa ajili ya kufanya tathimini mitihani ya darasa ya saba na kubaini baadhi ya changamoto zinazoikabili elimu Mkoani hapo.
Kikao hicho kimekusudia kupata majibu kutoka kwa maofisa hao kueleza sababu ya baadhi ya halmashauri kutofikia asilimia 90 ya ufaulu ambao ni lengo la mkoa huo.
Kwa mujibu wa takwimu za mkoa huo zinaonyesha halmashauri ya Ilemela ilifikia asilimia 98.3, Sengerema 97.1, Misungwi 96.6, Jiji la Mwanza 95.2, Magu 92, Ukerewe 85.4, Kwimba 84.6 na Buchosa 80.5.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kikao na maofisa hao, Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola alisema lengo ni kuweka mikakati na kutatua changamoto zilizopo ili kila halmashauri iweze kufikia asilimia 90 ya ufaulu katika mitihani ya kitaifa.
Ligola alisema katika mitihani ya majaribio iliyofanyika ngazi ya mkoa, baadhi ya halmashauri ziliweza kufikia asilimia 90 lakini nyingine zilifikia asilimia 80, hivyo kitendo cha kuwakutanisha maofisa elimu wilaya, kata na wakuu wa shule ni kutaka kuwa katika mstari unaofanana.
Ligola alisema Julai 17-18 mwaka huu kulifanyika mtihani wa mjaribio mkoa ambapo wanafunzi 68,356 kutoka shule za msingi 944 walitarajiwa kufanya lakini waliofanya mitihani hiyo ni 67,322 kati ya hao wavulana 31,789 mna wasichana 35,533 na asilimia 98.3.
Alisema wanafunzi ambao hawakufanya mtihani huo 1,034 kati ya hao wavulana ni 347 na wasichana 687 sawa na silimia 1.5, hivyo alisema kiwango hicho cha wanafunzi wasiofanya mtihani ni kikubwa na kinapaswa kutafutiwa suluhisho.
“Lengo la Serikali ni ufaulu uwe asilimia 100 kitaifa lakini hapa Mkoa wa Mwanza tulijiwekea malengo yetu yawe asilimia 90 au zaidi,sasa katika mitihani ya majaribio tuliyofanya ngazi ya mkoa baadhi ya halmashauri zimeonekana kutofikia lengo letu, sasa nimelazimika kuwakutanisha ili kila mmoja aseme kilichomkwamisha hali hiyo kujitokeza.
“Bila shaka kila mmoja atasema na baadaye tutajadiliana kuona wapi panatakiwa kurekebishwa ili mtihani ujao tuweze kufanya vizuri, kwa habati nzuri Mkoa wa Mwanza hali ya taaluma siyo mbaya hivyo matarajio yetu shule zilizofaya vibaya tutasikia sababu zao ni zipi na tutaelezwa wale waliofanya vizuri wao walifanya nini,”alisema.
Kwa upande wa Afisa Elimu Kata ya Nyamanoro Wilaya ya Ilemela, Iloze Ngereza alisema licha ya eneo lake kufanya vizuri katika mitihani ya majaribio lakini changamoto kubwa iliyopo ni utoro wa wanafunzi.
“Unajua walimu wanaweza kuwa wanafundisha vizuri sana lakini changamoto inakuja ya utoro wa wanafunzi, hawa watoro ambao hawahudhulii masomo kila siku wanajitokeza siku ya mitihani na ndiyo wanaofanya vibaya na kusababisha kushusha ufaulu.
“Ukichumnguza wale wanaokuwa wanahudhuhulia kila siku wanafanya vizuri lakini wanaangushwa na wale watoro, mfano katika kata yangu ukifuatilia watoro katika shule zote unakuta wanafikia kati ya 300 hadi 400, ndiyo maana tunafikia hatua tunawafuatilia sambamba na wazazi wao,”alisema.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bujingwa iliyopo Wilaya ya Kwimba, Mathias Tito amesema shule yake ni miongoni kwa shule zilizofanya vibaya hivyo kikao hicho kitasaidia kubadilishana mbinu zitakazofanya halmashauri zote kuwa katika mstari mmoja wa ufaulu wa asilimia 90 kama malengo ya mkoa yalivyoainishwa.
“Unajua shule yangu ipo katika mazingira mabaya, ipo mbali ambapo walimu wanasafiri muda mrefu lakini kama kungekuwa na nyumba za kutosha zingesaidia kuishi pale pale, hata hivyo wanapokuwa shuleni pale wanashinda njaa hii ni changamoto sana,’”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.