MWENGE WA UHURU WAWASILI BUCHOSA, KUKIMBIZWA KWENYE MIRADI 8 LEO
Mapema leo tarehe 16 Julai, 2023 Halmashauri ya wilaya ya Buchosa imepokea Mwenge wa Uhuru ukitokea Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo unatarajiwa kukimbizwa kwenye Miradi nane yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.1.
Akizungumza kwenye mapokezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Michezo Iseni, kata ya Nyanzebo Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Senyi Ngaga amesema wana ari nzuri na wamejiandaa vema kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kwenye miradi iliyotawanyika umbali wa Kilomita 75.
Mhe. Ngaga ameongeza kuwa, miradi mitatu inatarajiwa kuwekewa mawe ya msingi, miwili kufunguliwa, huku miwili ikizinduliwa na mmoja ambao utatembelewa kwa ajili ya kukaguliwa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Abdalla Shaib Kaim ametumia wasaa huo kuomba ushirikiano kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri hiyo hasa wakati wa ukaguzi wa miradi na nyaraka na akasisitiza juu ya muhimu wa uwepo wa vielelezo vya malipo kwenye miradi.
Pamoja na kukimbizwa kwenye miradi, Mwenge wa Uhuru ukiwa Buchosa utakagua shughuli mbalimbali za Upimaji Afya, Utoaji wa Elimu na Chanjo ya Uviko 19, Vipimo vya HIV pamoja na Elimu ya upingaji Rushwa na madawa ya kulevya pamoja na Elimu dhidi ya Lishe bora.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 inasema "Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.