MWENGE WA UHURU WAWASILI MWANZA, RC MTANDA AUPOKEA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo 06 Oktoba 06, 2024 ameupokea Mwenge wa Uhuru ukitokea Mkoani Geita tayari kwa kutembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 58 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 98.
Akizungumza kwenye mapokezi hayo yaliyofanyika kwenye kijiji cha Nyamadoke Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Mhe. Mtanda amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya 7 na Halmashauri 8 katika umbali wa zaidi ya kilometa 649.
Ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani Mwanza utaifikia miradi lukuki yenye viwango katika sekta za maji, elimu, afya, kilimo na miundombinu kwani Mkoa huo unaochangia pato la taifa kwa asilimia 7.2 una uchumi imara na kwamba wakimbiza mwenge wataishi kwa amani kwani kuna utulivu.
Akizungumzia masuala ya lishe, Mhe. Mtanda amesema Mkoa huo umeendelea kuimarisha kwenye eneo hilo kwa kutekeleza afua mbalimbali kama kutoa elimu na kuimarisha lishe bora kwa chakula cha watoto shuleni na imesaidia kupunguza ukondefu kutoka asilimia 3 mwaka 2017 hadi asilimia 1 mwaka huu.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amesema ubora wa miradi utaonekana kwenye thamani ya fedha zilizotumika na huo utakua ndio msingi wa ukaguzi na kwamba taarifa sahihi za miradi zitachagiza ushindi kwenye ukaguzi.
Wakati huo huo Mhe. Mtanda amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mhe. Seni Ngaga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kukimbiza mwenge wa uhuru kwenye halmashauri ya Buchosa leo Oktoba 06 2024.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu ni "Tunza mazingira, "Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.