MWENGE WA UHURU WAZINDUA MRADI WA UFUGAJI SAMAKI WA VIZIMBA NYAMAGANA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amezindua mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wa kikundi cha Vijana kinachojulikana kama Vijana Agro wenye thamani ya Tshs. Milioni 206 hadi kuanza uzalishaji.
Akizungumza na wananchi mara baada ya ukaguzi kwenye eneo la mradi huo uliopo katika mtaa wa Kisoko, kata ya Luchelele wilaya ya Nyamagana leo Oktoba 09, 2024 Mnzava ameipongeza Halmashauri ya Jiji hilo kwa kuwakopesha vijana hao 7 kiasi cha tshs. milioni 150 hali iliyowafanya wapate na kupelekea kutengeneza miundombinu.
Aidha, amewataka vijana hao kuweka nidhamu kwenye utekelezaji wa mradi huo ili waendelee kuzalisha na kuuza samaki ambao soko lake ni kubwa sana kwa sasa na akawataka kuhakikisha wanafanya marejesho ya mkopo huo illi vijana na makundi mengine waweze kupata mkopo pia.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mwenyekiti wa kikundi ndugu Christopher Gugu amesema mkopo huo pamoja na mtaji wao wa milioni 56 walizokua nazo hapo awali zimewasaidia kutengeneza vizimba 3 vikubwa, ununuzi wa boti na injini yake, mitumbwi 2, mashine 2 HP 15, tani 21.8 za chakula cha samaki, vifaranga pamoja na ujenzi wa stoo ya kuhifadhia chakula cha samaki.
Aidha, ametaja manufaa waliyoyapata kutokana na mradi huo kama kuongeza mapato ya kikundi kwani uvunaji wa awamu mbili na umewapatia milioni 86.4 na kuwafanya waanze kurejesha mkopo huo pamoja na kuongeza boti kutoka 3 hadi 6 na kwamba wameajiri vijana 6 nje ya vijana 7 waanzilishi.
Mwenge wa Uhuru Wilayani Nyamagana umetembelea mradi wa maji safi Butimba wenye thamani ya bilioni 71.9 unaotekelezwa na programu ya maji na Usafi wa mazingira ambapo baada ya ukaguzi kiongozi wa mbio hizo ameipongeza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira (MWAUWASA) kwa kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.