Katika kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na viwango elekezi viongozi wenye dhamana ya usimamizi wa miradi wametakiwa kufuata maelekezo ya miradi mbalimbali yanayotolewa kuhusu miradi hiyo ili kuepuka maswali mengi yanayoleta wasiwasi wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Sahili Geraruma mapema hii leo mara baada ya kukagua miradi inayopitiwa na Mbio za Mwenge Wilaya ya Misungwi.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Manawa ambapo amekuta Ujenzi ukiendelea katika mradi huo uliogharimu shilingi milioni 471.8, ndugu Geraruma amewataka wenye dhamana ya usimamizi wa miradi kufuata taratibu zilizowekwa.
"Viongozi na wasimamizi wote wa miradi, hakikisheni mnafuata taratibu zote zinazotakiwa kuhusiana na miradi ikiwemo kuomba kuongezewa muda pale,mnaposhindwa kukamilisha kwa wakati na siyo kukaa kimya,''amesema Geraruma.
Aidha,ameshauri na kuwataka Viongozi wa Halmaahauri hiyo kusimamia vizuri Miradi ambapo amepongeza baadhi ya Miradi hiyo ikiwa ni pamoja na Miradi ya sekta ya Afya, Elimu, Maji, Uwezeshaji Wananchi kiuchumi na Mradi wa Ujenzi wa Barabara.
Pamoja na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa kuhusiana na Miradi hiyo, Miradi iliyowekewa jiwe la Msingi, na kuzinduliwa ni pamoja na Ujenzi wa Shule ya Sekondari Manawa, Ujenzi wa Barabara ya Lami, Ujenzi wa Kituo cha Afya Usagara, Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Afya MacWish, Mradi wa usambazaji Maji wa Fella, Ujenzi wa Madarasa 8 katika Shule ya Sekondari Sanjo, na Mradi wa usafi wa mazingira na usafirishaji mizigo.
Hata hivyo,Miradi hiyo imetokana na mchango wa jamii shilingi Milioni 11.3 na Halmashauri imetoa shilingi Milioni 16.7 ambapo Serikali Kuu imechangia shilingi Bilioni 1.6 na wahisani wamechangia shilingi Bilioni 1.5 na Miradi yote inaendelea kutekelezwa na baadhi imekamilika.
Akihitimisha ukaguzi wa miradi Geraruma amewataka wenye dhamana ya miradi hiyo kuhakikisha wanafanya marekebisho katika mapungufu yote yaliyobainika wakati wa ukaguzi ikiwa ni pamoja na kufuata na kuzingatia kanuni taratibu za Ujenzi ili kukamilisha Ujenzi huo na kupata Miradi inayokidhi na yenye Viwango.
Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu kesho tarehe 14/7/2022 baada ya kukamilisha mbio hizo Wilaya ya Misungwi ukitokea Wilayani Kwimba ambapo umekimbizwa km 75.3 na kupitia miradi 7 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.12.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.