Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb), ameitaka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kuhakikisha wawekezaji wanaajiri wafanyakazi wenye sifa na taaluma stahiki ili kuongeza ufanisi wa miradi.

Akizungumza Januari 6, 2026, wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mwanza, Mhe. Chaya alitembelea viwanda vya Rofi Farming na Ziwa Steel vilivyopo wilayani Magu.

Amesisitiza umuhimu wa ajira zinazozingatia sifa za kitaaluma kwa vijana ili waweze kusimamia na kuendeleza miradi kwa tija.

Aidha, amewapongeza wawekezaji hao kwa mchango wao katika ajira na uchumi wa Mkoa wa Mwanza.

Kiwanda cha Ziwa Steel kimewekeza shilingi bilioni 65 na kutoa ajira zaidi ya 800, huku Rofi Farming kikiwekeza shilingi bilioni 9 na kuajiri zaidi ya vijana 150.

Mhe. Chaya pia aliwataka wawekezaji waliopo nchini kuwa mabalozi wa kuvutia uwekezaji zaidi, akiahidi ushirikiano wa serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Kwa upande wake Msimamizi wa Ofisi wa Rofi Farming, Bw. Neziah Mussa, ameomba serikali kusaidia upatikanaji wa malighafi kwa kuhamasisha wakulima kulima zao la soya kwa wingi.

Naye Msimamizi wa Rasilimali Watu wa Ziwa Steel Wakili Philip Sylvanus, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.