Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amelishauri Baraza la Taifa la Hifadhi ya usimamizi wa Mazingira Tanzania,NEMC kupitia upya baadhi ya Sheria zake za utunzaji wa Mazingira hasa za Kelele sumbufu ambazo zimekuwa kero kwa wananchi siku hadi siku.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha Baraza hilo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliokuwa unajadili uwepo wa matumizi ya mifuko ya Plastiki na Kelele sumbufu,Mhe.Malima amesema utoaji wa vibali kwa kumbi za starehe na nyumba za ibada usiozingatia Sheria na taratibu umechangia kusababisha kero kwa wananchi na ushahidi ni ofisi yake inayopokea malalamiko hayo kila uchao.
"Kelele sumbufu kwa kweli zinawatesa sana wananchi,kaeni pitieni vizuri Sheria zenu na ikibidi mkaziongezee adhabu zaidi,baadhi ya nyumba za ibada zinakiuka kabisa taratibu kwa kupaza sauti usiku kucha bila kujali athari zake kwa walio jirani,hii kwa kweli haikubaliki",amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kuhusu mifuko ya Plastiki Mhe.Malima ameishauri NEMC kuona namna ya kuwajali wafanyabiashara wadogo ambao wamekuwa wakitumia baadhi ya vifungashio vya plastiki kwenye bidhaa wanazouza kwa kuangalia mpango mbadala na kuboresha baadhi ya vibebeo ambavyo havitakuwa na madhara kwenye mazingira.
"Bwana Kayombo hii jaribuni mkae na kulitazama vizuri hasa utoaji wa elimu kwa wananchi,nakubali kuna baadhi ya vibebeo havistahili kama vifungashio kwenye pilipili au vitunguu lakini bidhaa kama Njegere ili imvutie mnunuzi ikiwemo kwenye kibebeo cha kuonekana ana uhakika wa biashara yake kutoka maana wafanyabiashara hawa wengi mitaji yao ni midogo hawana ubavu wa kuweka bidhaa zao kwenye vyombo maalum ",Mhe.Malima.
Aidha Mhe.Malima ameliahidi Baraza hilo la Mazingira kushirikiana nalo akiwashirikisha viongozi wa Kamati ya Amani Mkoani Mwanza kuzifanyia ukaguzi na kuchukua hatua baadhi ya nyumba za ibada zisizo na sifa na kugeuka kero kwa wananchi.
"Tupo hapa Mwanza kwa muda wa siku saba kufanya ukaguzi kwa wanaokiuka matumizi ya mifuko ya Plastiki na Kelele sumbufu,tunashirikiana na kamati ya ulinzi na usalama wale wote watakaobanika mkondo wa Sheria utawapitia ikiwemo kufunga kumbi za starehe na nyumba za ibada na kuwachukulia hatua kali ikiwemo kifungo,"Hamad Taimour,Meneja uzingatiaji Sheria NEMC
"Nimefurahishwa na Mhe.Malima kutuletea hapa ukumbini uthibitisho wa matumizi yenye usahihi na usio sahihi wa hivi vibebeo vya plastiki,sisi kama NEMC hii changamoto tumeiona na tutaifanyia kazi lengo ni kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama kwa faida yetu na vizazi vijavyo, bidhaa zote ambazo haziozi ardhini kuhakikisha hazitumiki",Jerome Kayombo,Meneja Kanda NEMC
Baraza la Taifa la Hifadhi ya usimamizi wa Mazingira Tanzania NEMC, lilipitisha sheria ya katazo la matumizi ya mifuko yote ya Plastiki mwaka 2019 baada ya kubainika inachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi na uharibifu wa Mazingira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.