Prof Mkenda ahitimisha ziara ya kikazi kanda ya ziwa, aridhishwa na utekelezaji wa miradi*
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolph Mkenda ameendelea na ziara ya siku tatu katika Mikoa ya kanda ya ziwa iliyojikita katika ukaguzi wa Miradi iliyo chini ya Wizara hiyo ambapo leo Julai 06, 2023 amefika Mkoani Mara akitokea Mkoani Mwanza.
Akizungumza na Uongozi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kwenye Kampasi ya Oswald Mang'ombe, Prof Mkenda amesema amefurahishwa na Ukarabati wa Miundombinu ya chuo hicho ambao umeonesha nia ya dhati ya kutaka kudahili wanafunzi mwanzo wa muhula wa mwaka 2023/24.
"Tumezunguka kote, tumekagua na kwakweli tumeridhika na nina imani kwamba tukienda hivi basi tutakua tayari kupokea wanafunzi kwa ajili ya masomo ndani ya mwaka huu wa masomo na niwape tu taarifa kuwa tayari wajumbe wa baraza la Chuo wameshapatikana ambapo Mhe. Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu ndiye Mkuu wa chuo hiki." amesema Prof Mkenda.
Amesema Serikali imeamua kutenga zaidi ya Bilioni 2.6 kwa ajili ya ukarabati huo ili kuinua Sekta ya Kilimo nchini na kwamba chuo hicho kitaleta alama isiyofutika kwenye mageuzi ya Kilimo na Teknolojia nchini na ametumia wasaa huo kutoa rai kwa Uongozi kuanza kwa vitivo vinavyobuniwa vizuri ili kutoa umahiri uliokusudiwa kwa vijana.
Akitoa salamu za Mkoa wa Mara, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Said Mtanda ameihakikishia Wizara ya elimu ushirikiano ili kuhakikisha kinakarabatiwa na kuwa chuo cha mfano nchini ikiwa ni katika kuenzi pia tunu ya asili ya Baba wa Taifa Hayati Mzee Nyerere na kwamba kitakapokamilika kitachochea ubunifu, umahiri katika sekta ya kilimo na hata Utalii katika ukanda huo.
Mhe. Jumanne Sagini, Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi ametumia wasaa huo kuishukuru wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwaletea Butiama Miradi mbalimbali kwenye wilaya hiyo na ametoa rai kwa Uongozi wa Chuo hicho kuhakikisha Ukarabati unaanza mara moja na kukarabati chuo kwa ubunifu.
"Katika zoezi la Ukarabati Mhe. Waziri tumezishirikisha taasisi za wenzetu kama vile VETA, TBA, Bonde la Ziwa Victoria, Halmashauri ya wilaya ya Butiama na Ruwasa ambao wametuhakikishia kuwa tutapata maji ya kutosha kuhudumia chuo hiki." Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lesakit Mellau
Naye, Prof. Msafiri Jackson ambaye ni Kaimu Mkuu wa Chuo Utawala, fedha na Mipango amebainisha kuwa Mradi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere Kampasi ya Butiama utasaidia kuimarisha mafunzo ya kujifunzia na Ufundi Stadi.
Katika wakati mwingine Prof. Mkenda amefika kwenye kijiji cha Rwamkoma na kukagua eneo Maalum ambalo itajengwa miundombinu ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere tawi la Butiama ambapo zaidi ya Bilioni 44.5 zitatumika chini ya Mradi wa Higher Education Econ. Trans (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.