Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema amefurahishwa na programu ya Wanawake na Samia inayolenga kutoa ujuzi na uwezo wa kusimamia fani mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi na kipato kwa Wanawake na Wasichana.
Mkuu wa Mkoa amesema programu hiyo ni muhimu na kisha kutoa wito kwa watoto wa kike kuchangamkia fursa hiyo ili wanufaike na sio kuishia kutazama tu, amesema kwa sasa kila kijana ana vyeti vya taaluma lakini ni wachache walioajiriwa na serikali hivyo kundi kubwa ambalo halijaajiriwa Serikali inalinasaidia kupata taaluma ya ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Mkuu wa Mkoa amebainisha hayo leo Jumamosi tarehe 27, Septemba 2025 wakati akizindua Programu ya Mafunzo ya Wanawake na Samia katika Mkoa wa Mwanza iliyofanyika katika Viwanja vya michezo VETA Mkoa wa Mwanza.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amesema anatamani kuona kunakuwepo na majukwaa ya Wahitimu kutoka Vyuo mbalimbali ili wasikilizwe na kisha kupewa elimu ya fani tofauti tofauti kwa kuwa serikali ina mikopo na mitaji hivyo wanaweza kupewa elimu ya kujiunga na vikundi ili waweze kunufaika na kuanza kuingiza kipato.
“Na hapa lazima tubadili fikra zetu, ukiwa unakaa unasema huwezi kufanya jambo hili kwa kuwa jambo hili sio nililolisomwa inakua ni kupoteza muda”. Mhe. Mtanda.
“Hapa Mwanza kuna vitu vingi na hata vijana wanaweza kujiunga na kuunda vikundi wakawa na wazo lao hata la kufanya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wakati wanasuburi ajira ambazo ziko kwenye fikra zao lakini waanze kujikwamua na kuchangia pato la Taifa.” Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Akisoma taarifa ya Programu hiyo, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mwanza Bw. Thomas Kasele amesema Programu ya Wanawake na Samia ni programu inayodhaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo lengo lake ni kuwawezesha wanawake kupata uwezo na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa ili waweze kujikwamua na umaskini.
“Mkoa wa Mwanza jumla ya Wanawake 2500 wamedahiriwa katika fani mbalimbali ambapo kwa VETA Mwanza ni wanawake 2200, VETA Kwimba 18 na Ukerewe 83”. Amebainisha Bw. Kasele.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.