Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoani humo amewataka Wakufunzi watarajiwa wa Makarani wa Sensa katika ngazi ya Wilaya kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kusikiliza mafunzo kwa nidhamu na umakini.
Ametoa rai hiyo leo katika nyakati tofauti alipofika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) na Chuo cha Ualimu Butimba kufuatilia Mafunzo yanayotolewa kwa Makarani wanaoandaliwa kwenda kuwa wakufunzi wa Makarani katika ngazi za wilaya kwa ajili ya Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Jumanne ya tarehe 23 Agosti, 2022.
"Ndugu mshiriki wa mafunzo haya simama imara hili ni zoezi la kizalendo hivyo jitoe sadaka kwa Taifa kwa uwezo wako wote ili ukidhi vigezo vya nchi, tusiuangushe Mkoa wa Mwanza tutulie na kuelewa kwa kina ili tukafanikishe zoezi la Sensa ya Watu na Makazi." Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa Sensa ya Watu na makazi inahitaji takwimu sahihi za watu na uchumi wao ili kuweza kuisaidia serikali kupanga mipango yake na kwamba itasaidia hata kupanga mgawanyo wa maeneo ya kiutawala kama Majimbo, Wilaya na Mikoa.
"Tafadharini sana Makarani wetu, Serikali imewaamini hivyo nawaomba msikilize kwa makini na mkayashike yale yote mnayoelekezwa hapa ili mkaweke historia nzuri kwenye kazi hii muhimu ya Kitaifa." Amesema Kanali Stanley Ngatunga, Mkuu wa Vikosi vya JWTZ Mwanza.
Awali, Mratibu wa Sensa Mkoa alifafanua kuwa Makarani 260 waliopo SAUT kwa mafunzo ni sehemu ya 402 wataokwenda kutoa mafunzo kwenye wilaya kuhusiana na Dodoso Kuu la Sensa, Madodoso ya jamii, mambo ya kufanya baada ya sensa, Dodoso la Makundi Maalumu na matumizi sahihi ya Vishikwambi kwa ajili ya zoezi la kuhesabiwa.
Hashim Kyombo, mshiriki kutoka wilaya ya Misungwi amebainisha kuwa wamepewa maarifa na mbinu za kuwasaidia kuhoji na kudadisi kwenye kaya na katika makundi mbalimbalina kwamba kwa Elimu hiyo waliyopata zoezi hilo litakwenda kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Naye Mwalimu Viviani Nyambui kutoka Kata ya Luchelele -Nyamagana ameishukuru Serikali kwa mafunzo hayo ambayo yamefikia zaidi ya asilimia 80 na kwamba watayatumia kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 inafanikiwa kwa ufanisi mkubwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.