Mhe.Rais Dkt.John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa 35 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) utafaokafanyika jijini Mwanza kwa siku tatu huku kilio kikubwa kwa halmashauri ni kunyang’anywa vyanzo vya mapato na posho za madiwani.
Akizungumza na waandishi wa habari , Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Gulamhafeez Mukadam alisema mkutano huo unatarajiwa hudhuriwa na wajumbe na viongozi waalikwa zaidi ya 700 ambapo mada na changamoto mbalimbali zinazozikabili halmashauri zote nchini zitawasilishwa na kujadiliwa kwa kina na kutoa mapendekezo kwa Serikali Kuu.
Mukadam alisema mkutano huo ambao wajumbe wake ni wakurugenzi wote nchini, mbunge mmoja kwa kila mkoa, madiwani na viongozi wengine waalikwa, utatoa fursa kwao kuileza Serikali hali halisi ya namna halmashauri zinavyofanya kazi katika mazingira magumu.
Pia alisema watatumia nafasi hiyo kuwasilisha kilio chao cha muda mrefu juu ya maslahi ya madiwani pamoja na viongozi wa Serikali za mtaa wakiwamo wenyeviti na wajumbe wao ambao wanafanya shughuli nzito ya kuwahudumia wananchi lakini mwisho wa siku wanaachwa patupu.
Mukadam alisema hivi sasa halmashauri nyingi zimeyumba kutokana na kukosa vyanzo vipya vya mapato lakini aliishukuru Serikali kuu kwa kutoa pesa kwa baadhi ya halmashauri pale inapojitokeza kuwapo na uhitaji wa lazima kama ujenzi wa zahanati.
“Kumbukeni ALAT ni umoja wa halmashauri ya miji na majiji Tanzania sasa tunapokuja kukutana hivi ni jambo kubwa sana ndio maana tumemwalika Mhe. Rais Magufuli ili tumwambie halisi halisi ilivyo huku chini, tutamweleza juu ya mabaya na mazuri yaliyopo ikiwa lengo ni kusukuma maendeleo ya halmashauri zetu.
“Madiwani tunayo madai mengi sana yakiwamo kupandishwa kwa posho zetu na hiki ni kilio cha muda mrefu sana, pia hivi sasa halmashauri zimenyang’anywa vyanzo vyake na zinafanya kazi katika mazingira magumu, ingawa lengo la serikali ni zuri kwamba fedha zote zikusanywe pamoja na zitakuwa zikirejeshwa kwetu.
“Utakumbuka posho za madiwani zinalipwa kutokana na fedha za ndani, sasa kama vyanzo vya mapato ndiyo hivyo tumenyang’anywa sasa inakuwa vigumu madiwani kupata stahiki zao kwa wakati, naweza kusema pendekezo letu ni kutaka mzigo huu ubebwe na serikali kuu, maana huku halmashauri zipo taabani.
Hata hivyo aliziomba halmashauri ambazo hazijawasilisha michango yao ziweze kufanya hivyo ingawa wanatambua kwamba mifumo ya pesa imefungwa.Aliongeza kuwa mkutano huo utaleta fursa kwa Mkoa wa Mwanza na kuwataka wafanyabishara kuchangamkia mwanya huo waweze kufaidika.
Alisema mpaka sasa wameanza kuwapokea viongozi mbalimbali wa Serikali na huku akiwataka wajumbe wa ALAT kujisajili katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kupatiwa vifaa ili kuondoa usumbufu siku ya mkutano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.