RAIS SAMIA AMETOA BILIONI 30 KUJENGA JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE MWANZA LENYE HADHI YA KIMATAIFA : RC MAKALLA
*Abainisha kuwa Mkandarasi ameshapatikana na ujenzi kuanza hivi karibuni*
*Asema ndege za mizigo mbioni kubeba samaki kupitia uwanja wa kisasa ulioboreshwa*
*Asema Serikali inapambana na uvuvi haramu na kuhamasisha ufugaji wa kisasa wa samaki*
*Awapongeza kwa uzalishaji na kuwaahidi ushirikiano mkubwa zaidi*
*Awataka maafisa uvuvi na biashara kukomesha masoko yenye samaki wasiotakiwa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amebainisha kuwa Serikali imeamua kuboresha uwanja wa ndege wa Mwanza kuwa wa kimataifa kwa kufanya upanuzi na ujenzi wa jengo la kisasa la abiria ambapo Mkandarasi wa kujenga jengo hilo kwa Bilioni 30 ameshapatikana.
Makalla amesema hayo leo disemba 05, 2023 alipofanya ziara kwenye viwanda vya Samaki vya Nile Perch Fisheries Limited na Tanzania Fish Processors Limited vya Jijini Mwanza na kubainisha kuwa baada ya upanuzi huo uwanja utakua wa kimataifa na mizigo itasafirishwa moja kwa moja kupitia uwanja huo kwenda ughaibuni.
Amefafanua kuwa pamoja na Serikali kuleta ndege ya mizigo, imeamua kujenga jengo la abiria la kisasa kwenye uwanja huo na kufanya upanuzi wa njia ya kupaa na kutua ndege na kwamba kwenye kutekeleza hilo tayari tathmini imefanyika ili kuwaondoa waliovamia eneo la uwanja kwa kuwafidia ili kuwa na mazingira salama ya kazi.
Vilevile, amebainisha kuwa katika juhudi za Serikali kuboresha sekta ya uvuvi, hivi sasa wanahamasisha uvuvi wa kisasa hususani kwa kutumia vizimba na kukomesha kabisa uvuvi haramu ili samaki waongezeke na kuweza kusaidia kukuza soko na viwanda vilivyopo mkoani humo na katika hilo masoko ya samaki wasiotakiwa yanakomeshwa.
"TANESCO niwasihi tuboreshe utoaji wa huduma zetu, uzalishaji ukipungua mapato ya nchi yatashuka, ajira kwa watanzania na mitaji pia utapungua hivyo ni lazima muangalie namna ya kuwafanya wenye viwanda wasikwame kwenye uzalishaji." Amebainisha Mkuu wa Mkoa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Ndugu Rupesh Mohan amesema wameanza uzalishaji mwaka 1992 huku wakikua kiuzalishaji kila mwaka hadi tani 15 kwa siku wanazozalisha sasa kutoka 10 na kwamba wamejipangia kufikisha tani 80 na kwamba wanalipa Bilioni 1.8 kutokana na kodi ya usafirishaji nje bidhaa.
Halikadhalika amefafanua kuwa wanatumia milioni 200 kulipa ushuru wa huduma, ushuru wa kampuni milioni 150 pammoja na kuchangia zaidi ya Milioni 200 kwenye mifuko ya kijamii kama NSSF, WCF kupitia wafanyakazi 440 walio nao pamoja na kodi zingine.
Meneja wa Kiwanda cha Tanzania Fish Processors Limited Godfrey Samwel amebainisha kuwa uzalishaji kwenye kiwanda hicho umepungua hadi tani 15 kutoka 120 ambazo kiwanda kina uwezo nacho kutokana na upungufu wa samaki ziwani hadi kupelekea kuwa na wafanyakazi 300 kwa uwiano wa 40% Ke na 60% Me kutoka 500 waliokuwepo 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.