Rais Samia atoa msaada wa chakula kwa vituo vya watoto waishio mazingira magumu Mwanza
Leo Januari 9, 2024 Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msaada wa chakula kwa vituo viwili vya watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi Mkoani Mwanza katika wilaya za Nyamagana na Ilemela ikiwa ni zawadi za Sikukuu za Krismasi na na Mwaka Mpya.
Akikakabidhi zawadi hizo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Daniel Machunda kwenye vituo vya Console kilichopo wilayani Nyamagana na Fonalisco kilichopo Ilemela kwa kila kituo ni mchele kilo 100,maharage kilo 100,mafuta lita 20,mbuzi 1,nyanya tenga 1,juice katoni 3 pamoja na biskuti maboksi 3 vyenye thamani ya Shs 1,700,000
Akizungumza na viongozi wa vituo hivyo pamoja na watoto hao Machunda amesema msaada huo wa Rais ni ishara ya kuendelea kuwakumbusha Serikali inawajali, inawathamini na kuwapenda hivyo wasijione wanyonge au kutengwa na jamii badala yake wadumu katika tabia njema na kuzingatia masomo ili waje kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi au wafanyakazi bora wa Taifa hili siku za usoni.
"Nipo hapa mbele yenu kuja kuwaletea salamu za Rais wetu ninazo wasilisha mbele yenu kwa niaba ya mkuu wetu wa Mkoa Mhe.CPA.Amos Makalla amewasihi sana muishi kwa upendo huku mkiwa na imani Serikali ipo nyuma yenu kwa shida na raha hivyo ni wajibu wenu muendelee kujibidiisha katika masomo yenu kama anavyosisitiza Rais wetu kila mmoja asome bila kikwazo chochote,"amesisitiza Machunda wakati akizungumza na watoto hao kwenye kituo cha Fonalisco.
Amebainisha Ofisi ya mkuu wa Mkoa kupitia Idara zake husika itaendelea kuwa bega kwa bega na vituo hivyo kuhakikisha zinatimiza ipasavyo malengo yao ya kuwalea watoto hao kwa kuzingatia mila na desturi zetu ikitambuliwa hao ni hazina ya Taifa.
Kituo cha Console kilichopo wilayani Nyamagana kina jumla ya watoto 17 na Fonalisco cha Ilemela kina watoto 101 huku baadhi yao wakiwa masomo ya elimu ya juu.
Rais Samia amekuwa na utaratibu wa kutoa zawadi kwa watoto wote waishio katika mazingira magumu wakati wa sikukuu zote kubwa hapa nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.