RAIS SAMIA KUJENGA KIVUKO KIKUBWA KOME- NYAKALILO : RC MAKALLA
*Rais Samia atoa Bilioni 8 kujenga kivuko hicho*
*Kivuko kikubwa kubeba watu 400, magari 22*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inajenga kivuko kikubwa cha kisasa kitakachosafirisha abiria na mazigo katika kisiwa cha Kome hadi Nyakalilo katika Halmashauri ya Buchosa- Sengerema.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Nyamiswi kisiwani Kome leo tarehe 16, Januari 2024 Makalla amesema Serikali imedhamiria kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa maeneo hayo na imeamua kutenga zaidi ya Bilioni 8. kwa ajili ya kujenga kivuko hicho.
Amesema kivuko hicho kinachotarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu kitakua na uwezo wa kubeba tani 170 na kwamba kitasaidia kusafirisha mazao, bidhaa za uvuvi, magari na watu kwa pamoja tofauti na sasa ambapo wanatumia kivuko kidogo ambacho hakikidhi mahitaji.
Aidha, ametumia mkutano huo kuwapongeza wananchi kwa kupata shule ya Sekondari ya kisasa ya Buhama ambayo itakua suluhu ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule na amewaagiza TANESCO, RUWASA na TARURA kushirikiana na uongozi wa shule hiyo kufikisha huduma hizo muhimu.
Vilevile, Mhe. Makalla amewataka wananchi kuachana na uvuvi haramu kwenye ziwa Victoria ili kulinda rasilimali za ziwa hilo na kuruhusu mazalia ya samaki kwa ustawi wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa kanda ya ziwa na amewataka wananchi kulinda amani baina yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.