RAIS SAMIA SULUHU KUFANYA ZIARA YA SIKU MBILI MKOANI MWANZA
*RC Makalla awakaribisha Wananchi kumpokea uwanja wa ndege*
*Asema ataongea na Wananchi kwenye Mkutano wa hadhara Nyamagana*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amebainisha ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Jumatatu 29-30, 2024 ambapo atazindua ugawaji wa Boti 55 na Vizimba vya Samaki 222 kwa wanufaika 989.
Makalla amesema hayo mapema leo Januari 26, 2024 wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa ukihusisha pia ujumbe wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Kufuatia ugeni huo Makalla amewakaribisha wananchi wa Mwanza na Mikoa ya jirani kufika kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza siku ya jumatatu kwa ajili ya kumpokea na kumlaki pamoja na siku ya jumanne kwenye uwanja wa Nyamagana.
"Tarehe 30 Januari, 2024 Mhe. Rais atazindua ugawaji wa zana za uvuvi za kisasa kwa ajili ya uvuvi endelevu vikiwemo Boti na Vizimba pamoja na kuzungumza na wananchi wa kanda ya Ziwa kwenye uwanja wa Nyamagana, hivyo basi nawaalika wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza." CPA Makalla.
Aidha, amefafanua kuwa Rais Samia baada ya kuwasili Mwanza siku ya Jumatatu atatumia barabara kuu ya kuelekea mjini hivyo wananchi wanaalikwa kumlaki barabarani kuanzia Sabasaba, Pasiansi, Bwiru na Kwenye mzunguko wa Ziro ili kumshangilia na kumlaki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.