Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewataka madiwani na wawakilishi kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania kuwa huru kutoa maoni yao kuhusiana na uboreshaji wa kanuni za ajira.
Hayo yamesemwa leo Aprili 24 2023 kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza Utawala na Rasilimali Watu Bw. Daniel Machunda wakati akifungua semina ya mchakato wa ajira katika utumishi wa umma na ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya kuboresha kanuni za uendeshaji wa shughuli za sekretarieti,amewataka washiriki husika kuzingatia kile watakachojifunza ili wakachangie ufanisi wa kazi kwa kupata Watumishi wenye weledi.
Sekretari ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeandaa semina hiyo ili kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu na miongozo yote ya ajira inazingatiwa ikiwa hichi ndicho chombo kilichopewa mamlaka kisheria kuwezesha upatikanaji wa watumishi katika utumishi wa umma.
"Sekretarieti ya ajira imeona ni jambo zuri kuwashirikisha na nyinyi wadau ili muwe huru kutoa maoni yenu ambayo yatapelekea kupata kanuni mpya zitakazo ongeza tija katika mchakato wa ajira". Amesema Bw. Machunda
Pia Bw. Machunda amewataka washiriki wa semina hiyo kuzingatia mafunzo yatakayotolewa na wawezeshaji ili iwe rahisi kwao kushiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni ambayo yataboresha kanuni.
Aidha naye Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma Mhandisi. Samweli Tanguye amesema wameandaa semina hiyo kwa ajili ya kujielezea kwa wadau jinsi wanavyoendesha amichakato ya ajira na kanuni wanazozitumia.
" Tupo hapa Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu na kujielezea kwa wadau wetu juu michakato ya ajira inavyoendeshwa na kuwaonesha michakato ya ajira na kanuni tunazozitumia ili na wao waweze kupata nafasi ya kutoa maoni yao". Amesema Mhandisi. Tanguye
Naye Diwani wa kata ya Bujora halmashauri ya wilaya ya Magu Mhe. Bunyanyakei John amesema Sekretarieti ya Ajira ikiyafanyia kazi maoni ya washiriki yataleta matokeo makubwa sana katika ajira.
"Kama sekretarieti ya ajira ikisimamia kweli maoni ya washiriki basi maoni hayo ambayo tutayatoa yataleta matokeo makubwa katika ajira". Amesema Mhe. John
Semina hiyo ya siku mbili inayofanyika ukumbi wa Maji House Jijini Mwanza, imewahusisha Madiwani, Wakuu wa Idara ya Rasilimali Watu kutoka Taasisi za Serikali na wawakilishi kutoka Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Tabora, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara na kigoma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.