Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg Elikana Balandya amefunga rasmi wiki ya Kudhibiti na Kuzuia magonjwa yasiyoambukiza,ajali na akili ya afya kwa kuwakumbusha Wananchi kuitumia vyema elimu waliyopata kuhusiana na magonjwa hayo.
Akizungumza leo na hadhara kwenye kilele cha Maadhimisho hayo kwenye uwanja wa CCM Kirumba,Balandya amesema takwimu za Kimataifa za mwaka huu zimeonesha bado Dunia inapoteza nguvu kazi nyingi kutokana na vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
"Takwimu za mwaka huu zimeonesha watu Milioni 41 wanapoteza maisha,ni lazima juhudi za makusudi zifanyike kupambana na tatizo hili"amesema kiongozi huyo mtendaji wa Mkoa.
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuielimisha Jamii kupitia maadhimisho hayo yanayofanyika nchi nzima kila mwaka Novemba hali ambayo itachangia kupunguza na hatimaye kutokomeza tatizo hilo.
Aidha amewakumbusha wananchi kuzingatia utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara na kuwacha tabia ya kwenda Hospitali ugonjwa unapokuwa umefikia hatua mbaya.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi,Kifua Kikuu,dawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza Mhe.Fatma Tawfiq amebainisha wao kama Bunge wataendelea kuishauri Serikali kuweka mkazo kupambana na kuongeza bajeti ili kukabiliana kikamilifu na maradhi hayo.
"Tunashukuru Serikali yetu ni sikivu na yenye nia ya kuboresha maisha ya Mtanzania, miradi mingi ya afya ipo kila kona ya nchi hii tuendelee kuiunga mkono kwa jitihada hizi" amesisitiza mbunge huyo wa viti maalum kutoka Mkoa wa Dodoma.
Huu ni mwaka wa nne Serikali inafanya maadhimisho hayo, mwaka huu Mwanza ukiwa mwenyeji Kitaifa ukipokea kijiti kutoka Mkoa wa Arusha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.