Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg Balandya Elikana ameahidi kutoa ushirikiano kwa bodi mpya ya Kampuni ya Huduma za Meli MSCL iliyozinduliwa rasmi leo Mkoani Mwanza ili iweze kutimiza malengo yake kikamilifu.
Akizungumza na wajumbe wa bodi hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi,Balandya amesema kutokana na Mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha biashara eneo la Afrika Mashariki na kati,huduma za usafiri wa majini ni kitega uchumi muhimu.
"Nichukue nafasi hii kuwahakikishieni bodi hii sisi kama Mkoa tuna kila sababu ya kuwapa ushirikiano hasa kwa kutambua Serikali ya ya awamu ya Sita ilivyoipa Mkoa huu miradi mingi ya Kimkakati yenye lengo la kusukuma mbele Maendeleo ya Wananchi"amesema Mtendaji huyo Mkuu wa Mkoa.
Amebainisha eneo la Maziwa yote matatu ya Victoria,Nyasa na Tanganyika nchi jirani za Malawi,Congo DRC na Burundi zinategemea sana mizigo yao kupitia kwenye Bandari zetu hivyo wajumbe wa bodi hiyo watambue jukumu walilonalo la kuifanya Kampuni hiyo kuwa bora kwa huduma na nguzo imara ya Uchumi wa Taifa letu.
Akizindua rasmi Bodi hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Uchukuzi Mhe.Atupele Mwakibete ametoa maagizo kadhaa kwa bodi hiyo ikiwemo usimamizi wa ujenzi wa Meli zilizopo Maziwa yote matatu,kusimamia ukarabati wa MV Lyemba na Mv Sangara pamoja na ubunifu wa Masoko.
"Serikali itanunua Meli mbili mpya za abiria itakayochukua watu 600 na tani 400 na ya mizigo itakayobeba tani 3000 zitakazotoa huduma Ziwa Tanganyika" amesisitiza Mhe.Mwakibete
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Meja Generali mstaafu John Mbung'o amesema ana imani na wajumbe wake wenye taaluma zinazoendana na shughuli za Kampuni hiyo hivyo huduma za MSCL zitazidi kusonga mbele.
Bodi hiyo ya Kampuni ya Huduma za Meli itakaa madarakani kwa muda wa miaka miatu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.