Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amewataka washiriki wa mafunzo ya tathmini ya ulemavu kwa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kutumia vyema mafunzo waliyopatiwa na kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Amesema hayo leo Mei 26, 2023 wakati akifunga mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Bima kwa Wafanyakazi (WCF) yaliyo wahusisha Madaktari 100 kutoka katika Mikoa ya kanda ya Ziwa ambayo yamefanyika Mkoani Kwanza.
"Nipende kutoa rai kwa washiriki wote kutumia vyema elimu iliyotolewa katika mafunzo haya ili kuwawezesha kufanya tathmini ya ulemavu kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu na hatimaye kuwasadia wanaopata ulemavu unaotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi na kuusaidia mfumo wa fidia kwa wafanyakazi kutimiza lengo la kutoa fidia stahiki na kwa wakati," amesema Mtendaji huyo wa Mkoa
"Nchi yetu na Dunia kwa ujumla imekumbwa na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na uharibifu wa mazingira kwa msingi huo ni wajibu wa kila mmoja wetu kutunza na kuhifadhi mazingira yetu, tuchukue hatua za makusudi za kuhakikisha kuwa mazingira yetu yanalindwa ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, na kuendelea na zoezi la upandaji miti katika maeneo yetu," ameongeza Ndg. Balandya.
Aidha Mkurugenzi wa Huduma na Tathmini wa (WCF) Dkt. Abdulsalaam Omar amesema mafunzo hayo kwa Madaktari yanakusudia kuusadia mfuko katika kufahamu asilimia za ulemavu na kutoa fidia stahiki na kwa wakati.
" Mafunzo haya yamejikita katika kuwawezesha madaktari kuweza kufanya tathmini lengo kwa ujumla ni kuongeza ufanisi wa kazi na kutoa huduma bora," amesema Dkt. Omar.
Naye Dkt. Paskalet Jumba mshiriki wa mafunzo kutoka Hospitali ya Rufaa Geita amewasihi washiriki wenzie kwenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa pia wanakwenda kuwaelemisha na wengine waliobaki katika vituo vya kazi ili waweze kuielewa elimu hiyo.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa muda wa siku 5 ambayo yalifunguliwa Mei 22, 2023 na mpaka sasa Madaktari 1585 kwa Nchi nzima wamekwisha kupatiwa elimu hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.