RAS BALANDYA AWAPONGEZA ICAP KWA USHIRIKIANO NA SERIKALI YA MKOA WA MWANZA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bwana Balandya Elikana leo Novemba 12, amewapokea na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Shirika lisilo la Kiserikali la ICAP kutoka nchini Marekani na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkoa wa Mwanza kwa kuwezesha ajira zaidi ya wafanyakazi 400 katika sekta ya afya.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea, Katibu Tawala amewashukuru Viongozi hao ambao ni Mkurugenzi wa Fedha wa ICAP kutoka Makao Makuu New York, Marekani, Bibi Amy Gustavsson, ambaye aliambatana na Naibu Mkurugenzi Mkazi wa ICAP Tanzania, Dkt. John Kahemele pamoja na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa shirika hilo nchini, Ndugu Godfrey Hoya kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha kinga dhidi ya kuzuia na matibabu ya Virusi vya UKIMWI Mkoani Mwanza.
Aidha Bwana Balandya amewashukuru kwa kuendelea kuhamasisha kutahiriwa kwa wanaume kwa hiari kati ya vijana wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka 29, na ameshuhudia idadi kubwa ya vijana wakijitokeza kuhudhuria kliniki hiyo ambayo imekuwa na umuhimu mkubwa katika kupunguza maambukizi na kusambaa kwa virusi vya UKIMWI.
"Ninaendelea kuwashukuru kwani kupitia ICAP, Tumeongeza idadi ya wahudumu wa afya katika vituo vya afya ili kuhakikisha tuna rasilimali watu na tunafanikiwa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi".
Kadhalika amesema ushirikiano wa ICAP umesaidia katika ufungaji wa nishati ya jua kwenye vituo vya afya 81, hali iliyopelekea kuwepo kwa usambazaji wa umeme wa uhakika na huduma kutolewa bila adha ya nishati muhimu ya umeme.
Kwa upande wake, Bibi Amy amemshukuru Katibu Tawala na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa ambao ICAP imekuwa ikiupata na ameahidi kuendelea kushirikiana na Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla ili kuboresha afya za wananchi na kufikia malengo ya kuimarisha huduma za afya nchini.
ICAP ni Shirika lililo chini ya Chuo Kikuu cha Columbia, linaendesha miradi mbalimbali ya afya Mkoani Mwanza inayolenga kupambana na UKIMWI na kifua kikuu kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na CDC.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.