RAS BALANDYA AYATAKA MABARAZA YA WAZEE KUJENGA MAADILI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana ameungana na Wazee wa Mkoa wa Mwanza katika Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili kwa Wazee Duniani na kuwataka Mabaraza yao kuanzia ngazi ya kata hadi Wilaya yawe imara kujenga Maadili.
Akizungumza na Wazee hao leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa waliokutana kujadiiiana changamoto zinazowakabili,Balandya amesema bado wazee wana mchango mkubwa wa kuyajenga maadili hasa kutokana na hali ya utandawazi ambayo sehemu kubwa ya vijana wameathirika nayo.
"Ndugu zangu wazee Serikali inaendelea kutambua mchango wenu haya Mabaraza mliyonayo yaanze kuwamulika miongoni mwenu ambao mtawaona wanakwenda kinyume na maadili na kuonesha mfano mbaya kwa jamii",amesisitiza Mtendaji huyo wa Mkoa
Amebainisha kuwepo kwa Mabaraza hayo na kuweka mikakati madhubuti yatasaidia kukomesha matendo maovu ambayo bado yanameshamiri ndani ya jamii.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa,Silas Wambura amesema changamoto ya huduma ya afya kwa wazee itapatiwa jawabu na mpango ujao wa Bima ya afya kwa wote,hivyo kuwataka kuwa na subira wakati utaratibu ukiendelea kufanyika kabla ya kuwa sheria.
"Katibu Tawala wa Mkoa siku hii ya kupinga ukatili kwa wazee Duniani,tunalitumia jukwaa hili kujadiliana changamoto zetu na kukumbushana pia majukumu yetu kwa jamii kama walezi",David Manamba,M/kiti Baraza la ushauri la wazee Mwanza.
"Wazee wenzangu hebu sasa tubadilike na kuwa vinara wa kukemea mmomonyoko huu wa maadili,hali siyo nzuri kwenye jamii matendo mengi machafu yanaendelea kufanyika tushikamane kwa pamoja na Serikali yetu ili tuwe na jamii iliyostaarabika",Leonidas Mtawala,Katibu wa Baraza la wazee Misungwi.
Baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha kuwepo na Siku ya Kupinga Ukatili kwa Wazee Duniani mwaka 2011.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.